Kauli ya CHADEMA baada ya Komu kutangaza kuondoka

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa CHADEMA John Mrema, amesema kuwa Mbunge wa Moshi Vijijini ameamua kutoa kauli hizo kwa kuwa haamini chama kinasimamia nini na kwamba analazimika kubaki ndani ya chama kwa kuwa anasubiri posho zake za Bunge na kiinua mgongo.

Mrema ameyabainisha hayo leo Machi 29, 2020, masaa machache tu tangu Mbunge wa Moshi vijijini Anthony Komu, alipotoa kauli ya kuwa ataondoka CHADEMA mara tu mhula wake wa Ubunge utakapoisha na kwamba atahamia NCCR Mageuza kwa kuwa chama hicho kina itikadi ya utu.

"Komu ametangaza kuwa yupo kwenye chama kwa sababu ya kusubiri mafao ya Ubunge na posho za Bunge la Bajeti, kwani amesema kuwa atajiondoa kwenye chama mara baada ya mhula wa Ubunge wake utakapomalizika, akishalipwa mafao yake,  kiufupi tumbo lake ndio linampa sababu ya kubakia ndani ya chama" amesema Mrema.

Aidha Mrema ameongeza kuwa chama hicho kitakaa vikao vyake na kitatoa taarifa rasmi kwa umma juu ya jambo hilo.