https://monetag.com/?ref_id=TTIb Kilimo bora cha binzari | Muungwana BLOG

Kilimo bora cha binzari

Zao hili asili yake ni Mashariki ya Mbali, na linalimwa zaidi katika mkoa wa Tanga, Kagera, Kilimanjaro, Morogoro na Zanzibar. Binzari hutumika kwa mapishi ya nyama, samaki na mapishi mengine kwa kuweka rangi yake ya njano. Hutumika zaidi na nchi za mashariki kama India; nchi za Ulaya hutumia kidogo sana.

Mahitaji na mambo muhimu katika uzalishaji

Hali ya hewa
Humea vizuri maeneo yenye kiasi cha joto la nyuzi 24-26 za sentigredi na huzalishwa maeneo ya mwambao.

Udongo
Udongo wenye rutuba na unaopitisha maji na usio na mawe au changarawe. Mahitaji ya mvua ni milimita 1200-2000 kwa mwaka. Epuka kusimama kwa maji shambani. Umwagiliaji unaweza kufanywa endapo maji hayatoshelezi. Binzari inafanya vizuri ikipandwa sehemu ya uwazi. Ingawa pia inaweza kuchanganywa na mazao mengine kama minazi.

Uchaguzi wa mbegu
Mbegu zinazotumika hapa nchini ni za kienyeji bado. Tunguu kubwa zenye ukubwa wa sm 2.5 hadi sm 3 hutumika kama mbegu. Kiasi cha tani 1.7 za vipando huhitajika kwa hekta. Tunguu za kupandwa zisihifadhiwe kwa zaidi ya mwezi mmoja kabla ya kupanda.

Nafasi ya upandaji
Nafasi ya kupanda ni sm 15-25 kati ya mmea na mmea na sm 25-30 kati ya mstari na mstari au sm 45-60 kati ya tuta na tuta.

Mahitaji ya mbolea
Matumizi ya mbolea hapa Tanzania si makubwa katika kilimo cha viungo. Tafiti zimeonesha kuwa binzari hazioneshi kufanya vizuri kwenye mbolea za viwandani. Mbolea za samadi zinaweza kutumika. Kiasi cha tani mbili hadi tatu za samadi kwa eka moja kinatosha.

Uvunaji
Uvunaji hufanywa kwa kutumia majembe au uma. Binzari huvunwa wakati majani yamegeuka rangi na kuwa njano au kahawia. Binzari isiyo na kambamba huvunwa kipindi cha miezi sita toka kupandwa na miezi 18 hadi 21 kwa binzari iliyokomaa kutegemeana na mahitaji ya soko.

Mavuno ya tani 7 hupatikana endapo binzari ikipandwa peke yake. Mavuno hupungua kiasi binzari ikipandwa mchanganyiko na mazao mengine kwa mfano mavuno ya tani 4.8 kwa hekta yatapatikana binzari ikipandwa na minazi.

Utayarishaji
Kabla ya kuhifadhiwa binzari zichemshwe kwa dakika 45 hadi saa moja ili kuondoa harufu yake ya udongo. Pia kuchemsha kunasaidia zikauke kwa pamoja. Binzari zichemshwe  mpaka kijiti kisicho na ncha kali kiweze kutoboa kwa urahisi.

Kisha ziepuliwe na  kuanikwa juani kawaida huchukua siku 10 hadi 15 ili zikauke kufikia kiasi cha unyevu (moisture content) 5% hadi 10%. Binzari pia yaweza katwa vipande vidogo vidogo ili kurahisisha kukauka. Baada ya hapo ziko tayari kutwangwa au kusagwa kwenye mashine za kusagia viungo au kuhifadhiwa kama zilivyo.

Mashambulizi ya wadudu na magonjwa
Tatizo kubwa ni ugonjwa wa ukungu unaosababishwa na vimelea vinavyoitwa Colletotrichum sp.na Glomerella cingulata. Dalili ni madoa ya kahawia kwenye majani ambayo husambaa na kisha jani hukauka. Magonjwa haya yanaweza kudhibitiwa kwa kupiga dawa za ukungu kama Dithane M-45 kila baada ya wiki mbili.

Masoko
Soko la binzari linapatikana ndani na nje ya nchi.. Zao hili huuzwa katika nchi za Uganda, Kenya, Uingereza, Ujerumani, Mashariki ya Kati, n.k. Binzari yaweza kuuzwa ikiwa mbichi (mara tu baada ya kuvuna), ikiwa kavu au baada ya kusagwa kulingana na mahitaji ya soko.



Ushauri: Wakulima wanashauriwa kukausha binzari kwa uangalifu ili kutoharibu ubora wake.