KMC yatafuna mfupa uliomshinda Simba yaichapa Yanga bao 1-0

Bao pekee la mshambuliaji Salum Aiyee limetosha kuipa KMC ushindi wa bao 1-0 na kuirudisha dunia Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kipigo hicho cha Yanga kimekuja siku nne tu tangu mabingwa hao mara 27 wa Tanzania Bara waonyeshe soka la kiwango cha juu na kuifunga Simba bao 1-0 kwenye Uwanja Taifa.

Mshambuliaji Aiyee ndio kwanza amerejea kutoka katika majeruhi ya muda mrefu alifunga bao hilo pekee katika dakika 62 akipiga shuti la chini lililomshinda kipa Mechata Mnata wa Yanga na kujaa wavuni.

Hii ni mechi ya tatu kwa Aiyee kuifunga Yanga alifanya hivyo mara mbili msimu uliopita akiwa na Mwadui mechi zote alifunga mabao.

Ushindi huo unaifanya KMC kufikisha pointi 30 na kupanda hadi nafasi 16, wakati Yanga ikibaki nafasi ya tatu na pointi zake 50, Simba inaongoza kwa pointi 71, huku Azam ikiwa ya pili na pointi 54.
Katika mchezo huo wachezaji wa Yanga walishindwa kuonyesha ile soka ya kiwango cha juu waliyoonyesha Jumapili dhidi ya Simba na kuwafanya KMC kuonenaka bora kimbinu.

Mechi hiyo imeonekana kuchezwa kwa mbinu nyingi kwani kila kocha ameonekana kuingia kwa kuwapa maelekezo wachezaji wake kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu.

KMC wao walianza na mfumo wa (4-1-3-2), iliwasaidia kuwa na nidhamu kubwa katika kuzuia kwani licha ya Yanga kutengeneza nafasi za kufunga bao, lakini walishindwa.

KMC licha ya kuonekana walikuwa vyema kwenye kuzuia mashambulizi ya Yanga ambayo yalikuwa yakipitia kwa Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima na Mapinduzi Balama walionekana kutokuwa vyema kwenye kutumia nafasi chache za wazi za kufunga.

Beki wa kulia wa KMC, Kelvin Kajiri alitengeneza nafasi mbili za kufunga ambazo mshambuliaji wao Hassan Kabunda alishindwa kuzitumia kwa kufunga bao.

Yanga walianza mfumo wa (4-4-2), walitengeneza mashambulizi mengi eneo la kati kati ambapo alikuwa akicheza Papy Tshishimbi na Feisal Salum pamoja na pembeni ambapo walikuwepo Balama na Patrick Sibomana.

Kutengeneza huko mashambulizi kupitia kiungo na pembeni Yanga walitengeneza nafasi tatu za kufunga ambazo mbili zilimkuta Nchimbi na moja Tshishimbi.

Dakika ya 24, Yanga wanafanya mabadiliko anatoka Adeyun Saleh ambaye aliumia na nafasi yake kuingia Ally Mtoni.

Mbali ya mabadiliko hayo kila timu ilikuwa na nidhamu pamoja na mbinu kwenye kushambulia na kuzuia jambo ambalo lilichangia kipindi cha kwanza timu hizo zikiwa suluhu.

Kipindi cha pili kilianza kwa wenyeji KMC kufanya mabadiliko dakika 52, walitoka Kabunda aliyeumia na kuingia James Msuva pamoja na Emmanuel Mvuyekule aliyechukua nafasi ya Mohammed Samatta.

Mabadiliko hayo yalionekana kuwa na tija kwa KMC haswa kutawala katika eneo la katikati ambapo kulionekana kuwa na utulivu na maelewano makubwa kati ya Mvuyekule na Ramadhani Kapalata.

Dakika 62, Aiyee aliifungia bao KMC la kuongoza baada ya update uliofanywa na walinzi wa Yanga wakizani kuwa ameotea.

Mara baada ya kufunga bao la kuongoza dakika 63, alitolewa na nafasi yake kuingia Charlse Ilanfia, dakika tano baadae nao Yanga walifanya mabadiliko alitoka Sibomana na kuingia David Molinga.

Kuingia kwa Mvuyekule alionekana kuwa na utulivu na utimamu wa katika eneo la kati kati mwa uwanja kwani aliweza kutawala eneo hilo mbele ya viungo wa Yanga na kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi.

Dakika 72, kocha wa Yanga, Luc Eymael alipewa kadi ya njano baada ya kuonekana kuwa na jazba huku akipinga maamuzi ya refa Elly Sasii.

Yanga walifanya mabadiliko ya tatu dakika ya 81, alitoka Feisal Salumu na kuingia Deus Kaseke.
Mabadiliko haya yalimfanya Haruna Niyonzima ambaye alikuwa anacheza kama namba kumi kushuka kucheza kiungo wa mshambuliaji na Kaseke kwenda kucheza winga.

Dakika ya 92, straika wa KMC, Ilanfia alikutana na nafasi ya wazi uso kwa uso akiwa na kipa wa Yanga, Metacha Mnata ambaye alitaka kumpiga chenga ila kutokana na umahiri wake alipangua na mpira kuwa kona.