Majaliwa aridhishwa na kituo cha karantini

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameeleza kuridhishwa na maandalizi yaliyofanywa katika eneo lililotengwa kwa ajili kuwahudumia watu watakaobainika kuwa na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19), Wilayani Kibaha mkoa wa Pwani.

Akizungumza na wananchi wilayani humo baada ya kukagua hospitali ya wilaya ya Kibaha ambayo imetengwa kwa ajili ya kuwahudumia watu watakaogundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabilia na COVID-19, ambapo kwa sasa watu wote wanaoingia nchini kupitia viwanja vya ndege, vituo vya mabasi na bandari lazima wapimwe na wanaogundulika kuwa na maambukizi wanawekwa kwenye maeneo maalumu kwa muda wa siku 14.

Waziri Mkuu amesema lengo la kuwaweka kwenye maeneo maalumu ni kuweza kuwapima kila siku na kujirishika kama hawana maambukizi kwani mtu anaweza kupimwa leo akaonekana yuko vizuri lakini ana maambukizi ambayo bado hayaonekani kwenye vipimo lakini katika kipindi cha siku 14 mtu akibainika hana maambukizi anaruhusiwa kwenda kujiunga na familia.

Amesisitiza wananchi waendelee kufuata maelekezo yaliyotolewa na Serikali kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuzuia mikusanyiko na kwa wale wanaosafiri kwenye usafiri wa umma wasibanane kila mtu akae kwenye kiti na kuongeza kwamba wananchi wanapokwenda kufuata huduma kwenye masoko wahakikishe wanapeana nafasi baina ya mtu mmoja na mwingine na kabla hawajaingia katika maduka wanawe mikono kwa sabuni na maji tiririka ili kujikinga na maambukizi ya corona.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeanza kuwachukulia hatua watu wote wanaopotosha kuhusu taarifa za ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19).

Aliyetangaza kuwa shule zinafunguliwa tumeshamkamata na atachukuliwa hatua. Hivyo Waziri Mkuu amewataka wananchi wajihadhari na taarifa zinazotolewa na watu ambao si wasemaji rasmi na kusisitiza kwamba taarifa kuhusu virusi vya corona itatolewa na Waziri Mkuu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Msemaji Mkuu wa Serikali.