Mali kufanya uchaguzi wa bunge licha ya janga la COVID-19

Mali inafanya leo uchaguzi wa bunge uliocheleweshwa kwa muda mrefu licha ya kitisho cha janga la virusi vya corona na wasiwasi wa usalama.

Uchaguzi huo unafanyika wakati jana nchi hiyo ilitangaza kifo chake cha kwanza kutokana na virusi hivyo.

Kutekwa nyara kwa kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Soumaila Cisse mapema wiki hii pia kumetia wingu jeusi kwenye zoezi hilo, huku duru ya usalama ikisema huenda yuko mikononi mwa kundi la wanamgambo wa itikadi kali.

Cisse mwenye umri wa miaka 70, alimaliza wa pili katika chaguzi tatu zilizofanyika awali. Vyama kadhaa vya upinzani jana vilitoa wito wa kuahirishwa uchaguzi huo kutokana na janga la COVID-19, ambapo watu 18 wameambukizwa nchini humo tangu kisa cha kwanza kiliporipotiwa Jumatano wiki hii.

Taifa hilo maskini la Afrika Magharibi lina idadi ya watu milioni 19.