Sababu za kufa kwa mahusiano mengi ya ndoa

Mapenzi ni kitu fulani tofauti sana kwenye hii dunia na hata nje ya hii sayari. Mapenzi kwa kiasi kikubwa sana yanasababisha hata mambo mengine kwenye hii dunia yaende sawa au yaende tofauti hata kama hayahusiani na mahusiano ya mapenzi.

Vifo vingi hutokana na mapenzi, kuna magonjwa watu wanaumwa kisa mapenzi, kuna mambo watu wanayafanya si ya kawaida kisa mapenzi.

Ukiachilia mbali PESA, Mapenzi huwa yana nafasi kubwa sana kwenye kitu chochote ndani ya hii dunia tunayoishi. Si masikini wala si tajiri, wote kwa pamoja wanahitaji mapenzi kutoka kwa wanaowapenda ili dunia iweze kwenda sawa kwa upande wao. Na ndio sababu hata mimi hapa ninaandika kuhusu mapenzi kwa sababu yananigusa hata mimi na hata wewe unayesoma hapa sasa.

Ukipata mpenzi anayekuelewa na kukupenda basi hata dunia iwe ya tabu vipi kwako utaiona inazunguka kama kawaida na maisha yatasonga mbele kwako kwa raha mustarehe, na hata matatizo mengine makubwa kwako huwa madogo kwa sababu tu unapenda na kupendwa kwa dhati.

Lakini ukiumizwa kwenye mapenzi au kutojaliwa kama wewe unavyojali basi hata dunia iwe na raha gani kwako utaiona chungu na hata raha ya maisha hutakuwa nayo hata kama una hela kiasi gani na hata kama una cheo kikubwa kama mfalme au hata rais. Wengine hufikia hatu ya kuteseka tu bila kuondoka kwenye mahusiano kwa kuogopa kuumizwa tena huko waendapo na wengine huondoka baadae sana wakiwa tayari wameshachelewa.

Kuna sababu nyingi sana zinazoweza kusababisha mapenzi kupungua kwenye mahusiano yenu na wakati mwingine hata kusababisha kuachana. Mojawapo kati ya sababu hizo ni pamoja na hizi zifuatazo;-

Uongo.
Hakuna kitu kibaya kama uongo kwenye mapenzi, uongo wa aina yoyote ile si mzuri kwa wanaopendana kwa dhati kwa sababu huweza kupunguza mapenzi na uaminifu kwa kiasi kikubwa sana miongoni mwa wanaopendana hasa kama mmojawapo akigundua kuwa mwenzi wake ni muongo/anamdanganya.

Kuna vitu vingine hata kudanganyana haileti maana wala haina tija kwa hiyo kuwa mkweli kwa mpenzi wako kwa lolote lile ni jambo jema sana kuliko kuwa unamdanganya kila siku hadi aje kugundua unamdanganya itakuwa matatizo na unaweza kusababisha kuachana.

Usiri uliopitiliza.
Miongoni mwa vitu hatari pia kwenye mahusiano ni pamoja na hili la usiri wa kupitiliza. Kama una vitu moyoni na upo kwenye mapenzi/mahusiano bora kabisa si vizuri kuvificha na hasa vile vinavyohusiana na mapenzi yenu moja kwa moja. Ni kweli kuna vingine huwezi kumwambia kwa sababu havina mahusiano ya moja kwa moja na mahusiano yenu ila kuna vingine ni lazima avijue ili kutoleta ugomvi au matatizo hao baadae.

Kama kuna kitu hukuwahi kumwambia na unahisi ukimwambia atakasirika ni bora umtafutie nafasi nzuri umwambie kuliko aje kugundua mwenyewe itakuwa shida sana kukuelewa, kwa mfano mpo kwenye mahusiano mwaka wa 4 sasa na kumbe kabla ya kuwa na yeye ulishawahi kuoa/kuolewa na una watoto 2 kwa huyo mke/mume wa mwanzo ni bora umwambie kuliko kumficha, anaweza kukuelewa lakini mara nyingi ni kwa shingo upande.

Dharau.
Hii pia huchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza mapenzi kama sio kuyamaliza kabisa. Unapokuwa kwenye uhusiano jitahidi kumpenda mtu wako kwa khali yoyote na usiwe na dharau kwake au hata kwa marafiki zake au ndugu zake au hata wengineo. Hakuna mtu anayependa mtu mwenye dharau hata awe nani.

Kukosa uvumilivu.
Tamaa ni kitu kingine ambacho hufanya mahusiano mengi kukosa nguvu na mengine kuvurugika kabisa. Kama mpo kwenye mapenzi na mmeamua kupendana kwa shida na raha basi haitakiwi mmoja wenu kuwa na tama na kukosa uvumilivu hata kwa yale mambo yanayoweza kuzuilika.


Kama mpenzi wako ni wa hali Fulani na umeamua kuwa naye basi usiwe na tama kwa vitu vingine ambavyo vinaweza kukusababishia mahusiano yako kukosa nguvu na kufa kabisa. Amini kuwa ipo siku mtakuwa na vitu kama unavyotamani kwa kuongeza bidii kutafuta na kushauriana nini cha kufanya lakini si kwa kutafuta ‘’shotcut’’/njia nyepesi nyepesi zinazoweza kuku-cost hapo baadae.

Kukosa msimamo.
Hii kitu huwakuta wengi sana kwenye mapenzi ya siku hizi. Nadhani ni hali halisi ya dunia ya sasa inachangia pia pamoja na teknolojia tuliyonayo ya kutuwezesha kufanya yale tunayoyaona kwenye mitandao na vyombo mbali mbali vya habari.

Wapenzi wengi siku hizi wamekosa msimamo kwenye mapenzi/mahusiano yao na unakuta tu mmoja anakuwa na wapenzi zaidi ya mmoja na wanakuwa hawafahamiani huku kila mmoja akijua kuwa yeye ndo kila kitu kwa mpenzi wake.