Simba Yamkomalia Mzambia wa Orlando Pirates

KAMA ulikuwa unachukulia ni utani Simba kumuhitaji Bernard Morrison wa Yanga, basi sikia hii, unaambiwa uongozi wa Simba ulikuwa na mapendekezo ya majina mawili mkononi ambapo walikuwa wakimuhitaji Morrison au Justin Shonga wa Orlando Pirates.

Sasa baada ya kumkosa Morrison ambaye amesaini mkataba wa kuendelea kuichezea Yanga kwa miaka miwili zaidi, sasa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara wamemkomalia Shonga mwenye uraia wa Zambia.

Simba chini ya Kocha Mbelgiji, Sven Vandenbroeck, wanafahamu kuwa ni wazi watashiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, hivyo wanahitaji mchezaji ambaye ataongeza nguvu katika kikosi chao haswa katika eneo la ushambuliaji ambapo kwa sasa eneo hilo linachezwa na washambuliaji wawili pekee, Meddie Kagere na John Bocco.

Chanzo cha kuaminika kutoka Simba kimelipa mchongo Spoti Xtra kwa kusema, uongozi wa timu yao ulifahamu wazi Morrison hakuwa na mkataba zaidi ndani ya Yanga baada ya msimu huu kumalizika, hivyo wakaanza kumnyatia kimyakimya.

Lakini baada ya wenyewe kushtukia mchezo na kumuongezea mkataba, basi wakaamua kuhamishia nguvu zao kwa mshambuliaji ambaye walikuwa washaanza mazungumzo naye, Justin Shonga.

“Uongozi wa Simba ulikuwa siriazi kabisa katika kuhakikisha wanamnasa Bernard Morrison, lakini wakati huohuo pia walikuwa wanajaribu kuona kama wataweza kumsajili mshambuliaji wa Orlando, Justin Shonga.

“Lakini baada ya kuona kuwa Morrison amesaini mkataba na Yanga, basi wameona itakuwa ni ngumu tena kumpata, hivyo wameamua kukaza kwa Shonga ambaye licha ya pesa inayohitajika kuanzia shilingi milioni 800, kuna uwezekano wa kupungua na kumnyakua mwamba huyo ndio maana mazungumzo yanaendelea.

“Unajua Simba haina matatizo mengi kwenye kikosi chake na kocha anahitaji wachezaji kama wanne tu wa kuboresha kikosi na mchezaji wa kwanza ambaye ni kipaumbele anayemuhitaji kocha ni mshambuliaji wa kati, hivyo mshambuliaji huyo wa Orlando Pirates anaweza akasajiliwa iwe isiwe,” kilisema chanzo.

Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa ambaye ni raia wa Afrika Kusini mwenye mamlaka ya kuzungumza mambo mengi ndani ya klabu hiyo, jana alitafutwa kuweka wazi suala hilo, lakini hakupatikana, viongozi wengine wakawa waoga kwa sababu siyo wasemaji mkuu kumzidi Senzo.

Mbali na Senzo kukosekana, hivi karibuni Sven alisema: “Wachezaji nilionao wengi wanashindwa kutumia vizuri nafasi za kufunga, hivyo ninahitaji mshambuliaji ambaye atakuwa na uwezo mkubwa wa kufunga.” Shonga mwenye umri wa miaka 23, alisajiliwa na Orlando Pirates mwaka 2017 akitokea Nkwazi FC ya Zambia kwa dau la shilingi milioni 383. Katika Timu ya Taifa ya Zambia kuanzia 2017 mpaka sasa, amecheza michezo 24 huku akifunga mabao 13