TALGWU Manyara yawapatia elimu wanachama wake Kujikinga na Corona


Na John Walter, Babati

Chama cha wafanyakazi  wa serikali za mitaa Tanzania  [TALGWU] Mkoa kimetoa mafunzo kwa watumishi wa kada ya afya  katika hospitali ya Dareda  iliyopo Wilaya ya Babati ili waweze kujikinga  na virusi vya COVID-19  wakati wanatoa huduma kwa wagonjwa.

Katibu  wa chama cha wafanyakazi wa serikali  za  mitaa Mkoa wa Manyara Ndulilah Pandauyaga akizungumza leo machi 26 katika mafunzo hayo, amesema kuwa chama hicho kimeamua kutoa elimu hiyo kwa watumishi wa afya kutokana na chama hicho kuwa na wanachama wengi kutoka idara ya afya hivyo endapo itatokea mlipuko wa ugonjwa huo kwa wataalamu hao chama hicho kinaweza kupoteza wanachama wengi.

Amesema kuwa wauguzi wakijilinda wakiwa na afya nzuri wananchi wanakuwa na matumaini makubwa ya kutibiwa kwa uhakika hivyo kutolewa kwa elimu hiyo itawasaidia .

Naye katibu wa afya wilaya ya Babati Suten Mwambulambo  alisema  kuwa ni  vyema Wataalamu wa afya  kujikinga wao na familia zao na  ugonjwa wa corona  na kuacha tabia ya kujitenga kwani wao pia ni binadamu na kwamba wanaweza kuathiriwa na ugonjwa huo  bila kujali taaluma zao.

Joseph Lorri  ni Mganga mkuu wa hospitali ya Dareda anaeleza kuwa mafunzo hayo yamewafanya wazidi kuwa makini katika kutoa huduma kwa umakini mkubwa na kujikinga na maambukizi dhidiya Corona.

Mafunzo hayo yalijumuisha watumishi wote wa hospitali ya Dareda,Wauguzi,Madaktari,Walinzi ,Mafundi pamoja na wafanya usafi.

Aidha alieleza kuwa barakoa na vitakasa mikono vimekuwa ni adimu kupatikana  kwa sasa lakini  awali kabla ya ugonjwa huu kuingia hapa nchini walikuwa nazo nyingi na zilikuwa zikitumika kwenye upasuaji  na watu wanaofanya usafi nje, baada ya ugonjwa kuingia ikaonekana  kila mtumishi anataka kuvaa  ndio shida ikatokea   na katika muda mfupi tukaishiwa

‘’Tumejaribu kutafta wale wanaosambazia  hivi vifaa  wanasema hazipatikani, na hatujui tunaenda kuzipatia wapi  na hata wakati mwingine ukizipata unakuta bei inaongezeka  siyo sawa na zamani walivyokuwa wakiuza’’  alisema.

Hata  hivyo mganga mfawidhi wilaya ya Babati Madama Hosea alikiri ni kweli  kumekuwa na upungufu wa dawa ikiwa ni pamoja na vitakasa mikono  na hivyo wanafanya mawasiliano na Bohari kuu ya madawa kwa ajili kupatiwa madawa na vifaa hivyo baada ya muda mfupi  vitaletwa kwani tayari wameshaomba.