Viongozi wa G20 kufanya mkutano kwa njia ya video

Viongozi wa nchi zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi, G20 wanafanya mkutano kwa njia ya video leo hii, kuzungumzia mbinu za kupambana na mripuko wa virusi vya corona, na kushughulikia matatizo ya kiuchumi yanayotokana na mripuko huo.

Mkuu wa Shirika la Afya Ulimenguni WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus atatoa ujumbe katika mazungumzo hayo, ambapo anatarajiwa kuomba msaada wa kuwezesha utengenezwaji wa vifaa vya kujilinda dhidi ya maambuki ya virusi vya corona, ambavyo vimeadimika.

Katika mkutano na waandishi wa habari jana mjini Geneva, Ghebreyesus alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa, katika kupambana na janga la virusi hivyo.

Virusi hivyo vimekwishawauwa watu zaidi ya 21,000 miongoni mwa 471,000
waliokwishaambukizwa kote duniani.

Mapema wiki hii, mawaziri wa fedha na wakuu wa benki kuu kutoka nchi hizo, waliweka mkakati wa kudhibiti virusi hivyo, lakini hawakutoa maelezo zaidi.