Waandishi watakiwa kuandika habari kuwaelimisha wazazi kuwalinda watoto wasipate corona


Na Baraka Messa, Songwe

WAKATI Shule zikiwa zimefunga hivi karibuni nchini kwa ajili jitihada za kupambana na ugonjwa hatari wa Coorona (Covid 19) waandishi wa habari Mkoani Songwe wametakiwa kuandika habari za namna ya kuelimisha wazazi na walezi kuwalinda watoto katika kipindi hiki ambacho shule zote zimefunga kutokana na wazazi wengi kutokuwa karibu na watoto licha Serikali  na watalaam wa afya kusisitiza hilo.

 Hayo yametolewa na mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Nicodemas Mwangela wakati akizunguka na kamati ya Ulinzi na usalama mkoa wa Songwe kukagua maeneo yaliyotengwa ikiwa wagonjwa watapatikana katika Halmashauri za Mbozi, Ileje na Tunduma ambapo alibaini mapungufu mbalimbali katika baadhi ya vituo vilivyotengwa.

Alisema lengo la Serikali la kufunga shule zote nchini ni kuhakikisha watoto wanakuwa sehemu sahihi na salama kwa kipindi hiki cha mlipuko wa Ugonjwa wa Corona ulimwenguni kote wakisimamiwa na wazazi ,walezi na jamii kwa ujumla ili kuwakinga watoto hawa wadogo hasa wale ambao wanasoma elimu ya awali na wenye umri mdogo zaidi.

"Waandishi wa habari tusaidieni kuwaelimisha hawa wazazi na walezi ambao bado hawajui majukumu yao ya kuwalinda watoto kwa kuzuia mikusanyiko , ambapo wengine bado wanawaacha watoto wao wakizurula ovyo pasipokuwa msaada kutoka kwa wazazi ,walezi na jamii kwa ujumla.

Pazeni sauti Waandishi wa habari huu Ugonjwa ni hatari lakini bado jamii zetu zinachukulia kawaida Ugonjwa huu ukiingia madhara yake ni makubwa , tuchukue tahadhari mapema kabla Ugonjwa huu haujafika katika maeneo yetu, Kama unaingia ukute tumejiandaa na kila Mwananchi awe na elimu ya kutosha ikiwa ni pamoja na kuwalinda watoto wadogo hasa ambao wapo majumbani baada ya shule kufunga hivi karibuni." Alisema Mwangela

Aidha aliwataka wazazi kutambua kuwa jukumu la kuhakikisha watoto hawazunguki ovyo kuwa ni  la kwao kwa kuwa walimu ambao walikuwa wanawategemea hivi sasa hawapo karibu na watoto tena kutokana na shule zote kufunga .

Sanjar na Hilo mkuu wa Mkoa pia amewataka walimu ambao wanaanzisha vituo vya kufundisha watoto kwa malipo kuacha mara moja na kusisitiza kuwa watakaobainika watachukuliwa hatua Kali za kisheria kutokana na Serikali kukataza mikusanyiko ili kuwakinga watoto na watanzania kwa ujumla.

Kwa upande wake kamishna msaidizi wa polisi mkoa wa Songwe George Salala alisema kwa kipindi hiki jeshi la polisi wapo kwenye kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mikusanyiko ya aina yoyote kuzuiliwa ili kuendelea kujikinga na maambukizi ya Ugonjwa wa Corona ambao ni ni rahisi Zaid kuenea kwa njia ya mikusanyiko ya watu, hivyo kudai kuwa wanachukua hatua kwa yeyote anayepelekea mikusanyiko kipindi hiki cha mapambano dhidi ya Corona.

Pia aliwataka madereva na wamiliki wa magari kuacha mara moja kujaza abiria kupitiliza Jambo ambalo hupelekea abiria kuwa katika hatari kubwa ya kupata Ugonjwa wa Corona kutokana na wanavyobanana ikiwa watapanda na mtu mwenye maambukizi hayo .