Wizara ya Elimu imetoa elimu kwa wafanya kazi wake


Na Thabit Madai

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said amesema Wizara yake imeamua  kuwapatia Elimu wafanyakazi wake juu ya kujikinga na virusi vya korona.

Amesema kutokana na kuenea kwa kasi kwa virusi hivyo duniani ipo haja ya kuwaelimisha watendaji wa Wizara hiyo ili waweze kufanyakazi kwa umakini.
 Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu  ya Afya katika viwanja vya Wizara hiyo Mazizini Mjini Unguja Mhe  Simai amewataka wafanyakazi hao kuwa makini pamoja na kuifanyia kazi elimu waliyoipata na kuwa mabalozi wazuri wa kuwaelimisha wengine ili kuweza kujikinga na maradhi hayo.

Nae Afisa mahusiano kutoka kitengo Cha Elimu ya Afya Bwana Ahmed Mohamed amesema virusi vya ugonjwa wa Korona husambaa haraka, hivyo ni vizuri kwa kila mmoja kuchukua tahadhari ya hali ya juu ili kuepuka maambukizo ya virusi vya korona.

Amesema virusi husambaa kwa kushikana au kugusa sehemu za vitasa, funguo, ambavyo alieathirika  aliaacha virusi huku maambukizi,na dalili zake ni kupata homa Kali na kifua kikavu, kuumwa na kichwa Sana na machofu mwilini.

Aidha amesema Serikali ya Tanzania imetangaza rasmi kwa kila raia atakaeingia nchini kutoka nchi iliopata maambukizi, lazima awekwe kwenye Maandalizi Maalum kwa muda wa siku kumi na nne.

Nao Wafanyakazi wa Wizara ya Elimu Zanzibar wameishukuru Wizara yao kwa  hatua waliochukua viongozi wao kwa kuwapa Elimu watendaji wake, ambayo imewasaidia  kujua Kinga na athari za virusi vya korona.

Aidha wametoa wito kwa wazazi kuwasimamia watoto wao juu ya kutozurura ovyo na badala yake kujisomea majumbani mwao ili kuwaepusha na maambukizi hayo.