IOC Yapata Hasara Ya Trilioni 2

KAMATI ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) imesema kuwa kuahirishwa kwa Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020 imewagharimu kiasi cha Dola za Marekani milioni 800 (sawa na Sh trillioni 2), imeelezwa.

Rais wa IOC, Thomas Bach alitangaza kiasi hicho cha fedha baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika jana. Hii ni mara ya kwanza kwa IOC kutangaza hadharani hasara waliyopata baada ya kuahirishwa kwa Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020 ambayo ilipangwa kufanyika mwaka huu, lakini sasa itafanyika kuanzia Julai mwakani.

Awali, Michezo ya 32 ya Olimpiki ilipangwa kufanyika Tokyo kuanzia Julai 23 hadi Agosti mwaka huu, wakati sasa michezo hiyo itafanyika kuanzia Julai 23 hadi Agosti 8 mwakani katika jiji hilo la Tokyo.

Aidha, kiasi cha Dola za Marekani milioni 150 (sawa na Sh bilioni 347) kimetengwa na IOC kwa ajili ya Mashirikisho ya Michezo ya Kimataifa (IF) pamoja na Kamati za Taifa za Olimpiki (NOC), lakini haijawekwa bayana jinsi zitakavyotumika fedha hizo au kiasi kitakachogawiwa.

IF zimeachwa hoi baada ya kuahirishwa kwa Michezo ya Olimpiki ya 2020 kwa sababu ya mlipuko wa janga la vurusi vya corona, na fedha hizo zinatarajia kuziba mashimo yaliyosababishwa na kutokuwepo kwa kipato chao, ambacho hupata kutoka IOC baada ya michezo hiyo. Bach alithibitisha kuwa IOC bado inafikiria kutoa malipo ya awali kwa mashirikisho hayo ya michezo ya kimataifa na fedha za msaada na hiyo haina maana kuwa watakataa kutoa misaada kwa IF wakati baadhi ya Mashirikisho yalikuwa katika michato ya kukopa.

Mashirikisho yenye maskani yake Uswisi yanastahili kupewa mikopo, wakati Mashirikisho 32 ya Michezo ya Kimataifa yaliyopo katika programu ya Tokyo yanaweza kupokea fedha hizo kutoka katika fungu la IOC.

Dola za Marekani milioni 650 (sawa na Sh trilioni 1.5) zitakwenda kwa mashirikisho hayo ya michezo baada ya kuahirishwa kwa michezo hiyo ya mwaka huu. Gharama zaidi zimekuja baada ya uamuzi wa kuahirisha Olimpiki kwa mwaka mmoja kutokana na mlipuko wa janga la corona, ambayo inatarajiwa kufidiwa na Japan kutokana na kuwa mwenyeji katika mkataba uliosainiwa na IOC mwaka 2013.

Bach alikataa kuelezea kuhusu madai ya hivi karibuni kuwa Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020, ambayo imepangwa kufanyika kuanzia Julai 23 hadi Agosti 8 mwaka 2021, haitafanyika hadi pale chanjo ya COVID-19 itakapopatikana.

“Sasa tunafanyia kazi kwa nguvu zote kwa ajili ya mafanikio ya Tokyo 2020 mwakani 2021 na tunataka michezo hiyo iwe salamakwa washiriki wote, “alisema.