Iran kufungua tena shughuli zake za kiuchumi


Iran imeanza kurejea kwenye shughuli zake za kiuchumi kwa kufungua maduka, misikiti na sehemu za kitamaduni wakati huu ambao nchi hiyo inaendelea kulegeza vikwazo ilivyoweka.

Rais Hassan Rouhani amesema makavazi na sehemu za kihistoria zitafunguliwa kesho Jumapili, wakati waislamu nchini humo wanaposhehereka sikukuu ya Eid ul Fitr inayoashiria kukamilika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Sehemu za makaburi ambako kulikuwa ndio kiini cha virusi vya Corona nchini humo zitafunguliwa mnamo siku ya Jumatatu.Rouhani amesema wafanyakazi wote watarudi kazini Jumamosi ijayo.

Wiki iliyopita, Rais huyo alisema migahawa itafunguliwa baada ya mwezi wa Ramadhan na halfa za michezo zitaendelea tena japo bila ya mashabiki.

Wizara ya afya nchini humo imesema zaidi ya watu 7,000 wamefariki kutokana na ugonjwa wa Covid 19 na watu zaidi ya 130,000 wamethibitishwa kuwa na virusi vya Corona.