Marekani yasema Urusi inawafadhili mamluki Libya



Jeshi la Marekani limeishutumu Urusi kwa kutuma ndege za kijeshi nchini Libya kuunga mkono mamluki wa Urusi nchini humo.

Hakukuwa na jibu la moja kwa moja la madai hayo kutoka kwa wizara ya ulinzi nchini Urusi kwa usimamizi wa majeshi ya Marekani barani Afrika (Africom).

Mapema mwezi huu ripoti ya umoja wa mataifa iliovuja ilizungumzia kuhusu mamia ya mamluki kutoka kwa kundi la kijeshi la kibinafsi la Shadowy Wagner linalotekeleza operesheni zake nchini Libya.

Urusi inaunga mkono jeshi la jenerali Khalifa Haftar nchini Libya.

Taifa hilo limetoa wito mpya wa kusitishwa kwa vita na kuanza kwa mazungumzo ya kisiasa.

Waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Sergei Lavrov alijadiliana mgogoro huo na mshirika wake jenerali Haftar kwa njia ya simu siku ya Jumanne, kulingana na wizara hiyo.

Aliambia Aguila Saleh Issa, spika wa bunge, kwamba kuna umuhimu wa mazungumzo ya kina yanayohusisha majeshi yote ya Libya na usitishwaji wa vita.

Urusi haijathibitisha uwepo wa mamluki wa kundi la Wagner nchini Libya .

Kumekuwa na ripoti nyingi - ijapokuwa sio kutoka kwa maafisa wa Urusi kuhusu kupelekwa nchini humo kwa mamluki wa Wagner nchini Syria, mashariki wa Ukraine na maeneo mengine yenye vita ikiwemo Jamhuri ya Afrika ya kati CAR.

Serikali ya Urusi imekana kushirikishwa na kundi hilo.

Kulingana na serikali ya muungano GNA inayotambulika na Umoja huo wa kimataifa , zaidi ya wapiganaji 1,000 wa kundi la Wagner walitoroka eneo moja kusini mwa Tripoli wakiabiri ndege za kusafirishia mizigo za Urusi baada ya kusukumwa nyuma na wanajeshi wa GNA.

Kuondoka kwao hakukuthibitishwa na jeshi la jenerali Haftar nchini humo Libyan National Army {LNA} lililo na kambi yake eneo la mashariki wala Urusi.


Taarifa ya jeshi la Marekani linalofanya operesheni zake barani Afrika siku ya Jumanne ilisema: Moscow hivi majuzi ilipeleka ndege za kijeshi nchini Libya ili kulisaidia jeshi la Urusi la kibinafsi linaloungwa mkono na serikali ya Urusi linalotekeleza operesheni zake ardhini, lilisema.

Ndege hizo za kijeshi kutoka Urusi ziliwasili nchini Libya , kutoka kambi moja ya kijeshi nchini Urusi, baada ya kupitia Syria ambapo inadaiwa zilipakwa rangi ili kuficha chimbuko lake la Urusi.

Uturuki inaunga mkono jeshi linalotambulika na Umoja wa Kimataifa la GNA mjini Tripoli, na kulingana na gazeti la al Sabah nchini humo ndege nane za Urusi aina ya MiG-29 na Su-24 zilisafiri kutoka Syria kuelekea Libya ili kusaidia jeshi la jenerali haftar.

Ripoti hiyo ilimnukuu waziri wa maswala ya ndani wa GNA Fathi Bashagha.

Jenerali wa jeshi la Marekani Stephen Townsend, wa jeshi la Africom alisema: Ni wazi kwamba Urusi inajaribu kuingia katika vita hivyo kwa manufaa yake binafsi.....kwa kutumia kundi la mamluki wanoungwa mkono na serikali.

''Tulitazama huku urusi ikituma ndege za kijeshi za kizazi cha nne nchini Libya - kila hatua.

Hakuna jinsi jeshi la jenerali Haftar ama kampuni za kijesi za kibinafsi zinaweza kuwapatia silaha , na kuwawezesha kufanya operesheni na kuwalipa wapiganaji hawa bila kuungwa mkono na serikali. Wanaungwa mkono na Urusi'