Saudia Arabia ndio mnunuzi mkubwa wa silaha duniani


Kwa mujibu wa vyombo vya habari, utawala wa Saudi Arabia bado unashikilia nafasi ya kwanza kwa ununuzi wa silaha duniani.

Mtandao wa intaneti wa Al khaleej Online umeandika kwamba, tangu mwaka 2015 hadi 2019 serikali ya Saudia ilihodhi asilimia 12 ya uagizaji silaha duniani na kati ya nchi nne ambazo zinanunua silaha kwa wingi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, utawala wa Saudia pia umetenga asilimia nane ya pato lake la ndani kwa ajili ya gharama za kijeshi, kama ambavyo khumusi moja ya mauzo ya silaha za Marekani pia hutoka Saudia.


Mtandao wa huo wa Al khaleej Online umeongeza kwamba tangu mwaka 2015 hadi 2019 Saudia ilitiliana saini na Uingereza mikataba kadhaa ya mauzo ya silaha yenye thamani ya pauni bilioni 15 (sawa na dola bilioni 19).

Taarifa hiyo imeendelea kubainisha kwamba, mwezi Machi mwaka huu pia Saudia ilitiliana saini na serikali ya London mkataba wa thamani ya pauni bilioni tano (sawa na dola bilioni sita) na hivyo kuifanya Riyadh kuwa mnunuzi mkubwa zaidi wa silaha duniani. Mtandao huo umezidi kufafanua kuwa, kando na Marekani na Uingereza, utawala wa Aal-Saud pia umetiliana saini na nchi za Canada, Ujerumani na Russia kwa ajili ya kununua silaha.