Tanzania yaingia siku 17 bila taarifa ya corona

TANZANIA Bara, leo Jumamaosi tarehe 16 Mei, 2020, imeingia siku ya 17 bila ya taarifa za mwenendo wa hali ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu, inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19).

Mara ya mwisho taarifa za mwenendo wa ugonjwa huo, zilitolewa na Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania, tarehe 29 Aprili, 2020.

Siku hiyo, Majaliwa alitangaza ongezeko la wagonjwa wapya 167 wa Covid-19 ambao waliifanya nchi hiyo ianayounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kufikisha idadi ya wagonjwa 480 na vifo 16.

Hata hivyo, tarehe 7 Mei, 2020 Zanzibar ilitoa takwimu za mwenendo wa Covid-19 visiwani humo, ambapo Hamad Rashid Mohamed, waziri wake wa afya, alitangaza ongezeko la wagonjwa wapya 29 na vifo vitano.

Hiyo iliifanya Tanzania kwa ujumla kuwa na wagonjwa 509, vifo 21 na waliopona zaidi ya 183.

Tarehe 8 Mei, 2020, Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, alisema Tanzania imesimama kutoa takwimu hizo, kutokana na Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, kufanyiwa marekebisho.

Waziri Ummy alisema takwimu hizo zitaanza kutolewa tena, baada ya maboresho hayo kukamilika, huku akisisitiza hayatachukua muda mrefu.

Maboresho ya maabara hiyo, yalianza kufanyika siku chache baada ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kuangiza uchunguzi ndani ya maabara hiyo baada ya sampuli za wanyama na matunda kupimwa na kubainika kuwa na corona.

Kiongozi huyo wa Tanzania, alitoa tuhuma hizo, baada ya kueleza, vyombo vya usalama vilituma sampuli za baadhi ya vitu ikiwemo wanyama, ndege na matunda katika maabara hiyo, bila wahusika kujua, kwa ajili ya kuthibitisha ufanisi wa upimaji wa Covid-19.

Rais Magufuli alitoa maagizo hayo tarehe 3 Mei, 2020 wakati akimwapisha Dk. Mwigulu Nchemba, kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, hafla iliyofanyikia nyumbani kwake, Chato mkoani Geita.

Baada ya Rais Magufuli kueleza changamoto hizo, tarehe 4 Mei, 2020 Waziri Ummy, alimwagiza katibu mkuu, wizara ya afya, kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Dk. Nyambura Moremi na Jacob Lusekelo, Meneja Udhibiti wa Ubora,  ili kupisha uchunguzi.

Pia, aliunda kamati ya wataalamu wabobezi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa mwenendo wa maabara hiyo, ikiwemo mfumo mzima wa ukusanyaji na upimaji wa sampuli za Covid-19.

Kamati hiyo ya watalaam nane wabobezi, wakiongozwa na Prof. Eligius Lyamuya, kutoka Chuo Kikuu cha Afya Shirikisho Muhimbili (MUHAS), ilitakiwa kuwasilisha kwa waziri wa afya, taarifa ya uchunguzi huo kabla ya terehe 13 Mei, 2020.

Lakini hadi; leo tarehe 16 Mei, 2020 mamlaka husika hazijatoa taarifa yoyote juu ya matokeo ya uchunguzi huo.

Hata hivyo, jitihada za kumpata Waziri Ummy kuzungumzia mwenendo wa taarifa za corona na uchunguzi wa kamati aliyoiunda hazikuzaa matunda kwani simu yake ya kiganjani ilikuwa ikiita pasina kupokelewa.