Mapacha watatu waliozaliwa wapatikana na corona Mexico


Mapacha watatu Mexico wamepatikana na virusi vya corona hiki kikiwa ni kisa cha kwanza, kulingana na mamlaka ya afya ya eneo.

Wataalamu wa afya wanachunguza ikiwa watoto hao waliambukizwa kupitia kondo la nyuma la mama wakati wa ujauzito.

Wawili kati ya watoto hao mvulana na msichana, hali yao ya afya imeimarika lakini mvulana wa pili bado anapokea matibabu ya matatizo ya upumuaji, katika hospitali moja jimbo la San Luis Potosí.

Msemaji wa kamati ya masuala ya afya amesema magonjwa ya maambukizi kwa watoto wanaozaliwa bado haijawahi kutokea kokote kule duniani na hivyo basi hali hii inachunguzwa.

Ni idadi ndogo tu ya watoto wachanga ambao wamepata maambukizi ya virusi vya corona baada ya kuzaliwa lakini maafisa wa afya wanaamini kwamba hali haikuwa hivyo kwa mapacha hao watatu.

Waziri wa Afya Mónica Liliana Rangel Martínez amesema: "Haiwezekani kwamba waliambukizwa wakati wanazaliwa."

Hata hivyo wazazi wao wanapimwa virusi vya corona huku mamlaka ikisema huenda ni wale wagonjwa wasioonesha dalili.

Mexico imerekodi maambukizi zaidi ya 185,000 ya virusi vya corona na vifo 22,584 tangu nchi hiyo iliporekodi mgonjwa wa kwanza wa virusi hivyo Februari 28 .

Virusi vya corona kwa watoto wanaozaliwa

Mapacha hao - walizaliwa kabla ya muda, Juni 17 huko Mexico - na wote wakapatikana na virusi vya corona siku waliyozaliwa.

Virusi vya corona kwa watoto wachanga sio jambo la kawaida, kiasi kwamba haijawahi kutokea kabisa.

Watoto wanaweza kupata virusi vya corona baada ya kuzaliwa ikiwa watachangamana kwa karibu na yeyote ambaye tayari ameambukizwa virusi vya corona.

Virusi vya corona pia vinaweza kusambazwa hadi kwenye tumbo la uzazi kutoka kwa mama hadi kwa mtoto kupitia kondo la nyuma.

Watafiti Marekani kutoka Shule ya Tiba ya Yale hivi karibuni walitangaza maambukizi ya kwanza ya virusi vya corona kutoka kwa kondo la nyuma la mama.

Maambukizi yanapotokea, hatari ya kusambaa kutoka kwa mama hadi kwa mtoto iko chini sana, ingawa baadhi ya utafiti unaonesha kwamba yanaweza kuongeza uwezekano wa watoto kuzaliwa kabla ya muda.

Hakuna ushahidi unaoonesha kuwa virusi vinasababisha mimba kuharibika au kuathiri vile mtoto anavyokua wakati wa ujauzito lakini kama tahadhari, wanawake wajawazito wanashauriwa kuwa makini kabisa kutokaribiana na wengine ili kupunguza uwezekano wa kupata virusi vya corona.

Ikiwa watapata maambukizi, kina mama wengi wajawazito watakuwa na dalili za wastani au kawaida tu na kupona.

Watoto huenda wasioneshe dalili zozote za kupata maambukizi. Ikiwa una mtoto mdogo unaweza kupunguza hatari ya wao kupata maambukizi ya virusi vya corona kwa kuhakikisha mikono yako ni safi kwa kunawa kila mara.