Tume ya haki za binadamu ina jukumu kubwa la kulinda haki za wanawake na watoto-Balozi Seif


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ameitaka Tume ya Haki za Binadamu Tanzania kufanya wajibu wake wa kuwaelimisha wananchi kuhusu haki ili kuelewa haki zao pindi wamapokuwa na matatizo mbalimbali ya kijamii kwa kufanya kazi kwa karibu Serikali na kutekeleza majukumu yake kwa lengo la kuwatumikia vyema Wananchi wa  Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza Ofisini kwake Vuga Mjini  Zanzibar alipotembelewa na ujumbe wa Tume hiyo wakiongozwa na Mwanyekiti wake, Jaji Mstaafu Mathew  Pauwa Mhina, alisema, Zanzibar imekuwa na matukio mengi ya unyanyasaji wa kijinsia jambo ambalo Tume ya Haki za Binadamu inapaswa kuwaelimisha wananchi kuhusu upatikanaji wa haki pamoja na wakuwaeleza madhara ya unyanysaji wa kijinsia, kwani kufanya hivyo kutaisaidia Serikali kuu kupata nguvu na uwezo wa ziada wa kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili Wananchi hususan Wanawake, Watoto na hata Wananchi wenye mahitaji Maalum.

“ Tume ya Haki za Binadamu ina kazi kubwa katika kutekeleza majukumu yake  kwa upande wa Zanzibar kutokana na migogoro na changamoto nyingi zinazowakabili Wananchi hali inayosababisha mitafaruki na mifarakano miongoni mwa Jamii yenyewe, kwa hiyo nyie kama tume waelimisheni wananchi wa Zanzibar kufahamu sehemu ya kupata haki zao, lakini pia nyie mna jukumu kubwa la kusaidia kutatua migogoro na mifarakano inayotokea ya wananchi  kusumbuliwa  katika maeneo tofauti Nchini ” Alisema Balozi Seif .

Aidha , Balozi Seif aliueleza Uongozi wa Tume ya Haki za Binadamu kwamba yapo matatizo mengi yanayowakabili Wananchi hasa Wanawake ya kupewa ovyo Talaka na matokeo yake kutelekezwa na waume zao sambamba na kuachiwa  watoto bila ya huduma hali ambayo inakuwa ni kazi kwao kutimiza majuku ya kulea watoto.

Alitahadharisha kwamba tabia hii iliyoanza kuota mizizi kwa baadhi ya Wanaume wasiojali utu wa Binadamu ni ya hatari kwa Mtoto kwa vile inawakosesha haki zao za Msingi kama vile kupata elimu na huduma za Afya kwa sababu ya kutokuwa na ushirikiano wa kimalezi baina ya pande mbili.

Pia alieleza  suala  la  udhalilishaji wa wanawake na watoto  linaloikumba Dunia, hivyo watendaji na Viongozi wa Tume ya Haki za Binadamu lazima wajikite zaidi kushirikiana na Taasisi za utoaji haki pamoja na Wananchi katika vita ya kukabiliana na tatizo hilo linalochangia kupotoshwa kwa Maadili ya Jamii.

“Kwa sasa masuala ya wanawake na watoto kudhalilishwa limekuwa ni jambo ambalo duniani kote ni mtihani , kwa hiyo Tume ya Haki za Binadamu jikiteni zaidi katika kufanya upembuzi wa suala hili, ili Taasisi za utoaji haki na Serikali ipate kuwasaidia wananchi kupitia nyinyi, lakini pia misisahau kutoa elimu kuhusu haki zao kwani hiyo pia itawasaidia kupambana na waharifu na wavunjaji wa haki za Binadamu”, Alisema Balozi Seif.

Akijibu ombi la  Tume ya Haki za Binaadamu la kupewa jengo la Ofisi kwa upande wa Zanzibar,  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushauri ujumbe wa Tume kuwa na mpango wa kujenga majengo ya kudumu ya Ofisi zake Visiwani Zanzibar kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa maeneo ya ujenzi huo wakati wowote pale itapohitajika kutekelezwa mpango huo.

Kwa upande wake,  Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu Tanzania Jaji Mstaafu Mathew Pauwa Mhina, alisema Taasisi hiyo ni Chombo cha Umma kilichoundwa kusimamia upatikanaji wa Haki za Binadamu ili kusimamia Utawala Bora hapa Nchini na kuwawezesha wananchi kupata haki zao za msingi pale inapohitajika

“Tume  ya haki za binadamu imeundwa na viongozi wake waliteuliwa na Mhe Rais John Pombe Magufuli ili kutetea haki za Watanzania bila kujali imani zao, kwa hiyo utekelezaji wa majukumu yake upo kwa ajili ya wananchi wanaopokonywa haki zao, lakini pale ambapo watandaji wa Tume wakienda tofauti ni masuala ya kibinadamu ya kuteleza  katika Utekelezaji wa majukumu yao, hivyo Viongozi Wakuu wanapaswa kushauri pale Watendaji hao wanapoteleza katika maeneo yao ya Kazi”, Jaji Mstaafu Mathew Mhina.

Aidha Tume ya Haki za Binadamu Tanzania kupitia Mwenyekiti wake iliipongeza Serikali ya Jamahuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa  inayoifanya ya kuhudumia wananchi jambo ambalo uongozi wa Tume hiyo unaliunga mkono.

Makamishina wa Tume ya Haki za Binadamu Tanzania waliteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli mnamo Tarehe 19 Septemba Mwaka 2019, ili kuhakikisha kunakuwepo na upatikanaji wa haki kwa watanzania katika maeneno yote ya Kijamii.