Uingereza yajitolea kuwapokea raia wa Hong Kong

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema nchi yake iko tayari kuwafungulia milango raia wapatao milioni 3 wa Hong Kong wakati kiongozi wa jimbo hilo la China akiwasili mjini Bejing leo kwa ajili ya kushiriki mikutano kuhusu sheria ya usalama wa kitaifa iliyoandaliwa ambayo inawatia wasiwasi watu wengi kuhusu mustakabali wao.

Waziri mkuu wa Uingereza amesema kupitia makala iliyochapishwa mtandao na gazeti la Hong Kong linaloitwa South China Morning Post, kwamba sheria hiyo ya usalama itaweka rehani uhuru wa jimbo hilo na kwenda kinyume na wajibu wa China chini ya makubaliano yake na Uingereza wakati ilipokabidhiwa tena jimbo hilo mwaka 1997 kutoka mikononi mwa nchi hiyo ya Uingereza iliyokuwa inalitawala.

Boris Johnson amenukuliwa akisema kwamba ikiwa China itaendelea kuhalalisha hofu yake basi Uingereza haiwezi kuwapa kisogo watu wa Hong Kong.