Wilaya ya Njombe yaagizwa kuwachukulia hatua watendaji wanaosababisha hoja za mkaguzi



Na Amiri kilagalila, Njombe.

Halmashauri ya wilaya ya Njombe imeagizwa kuwachukulia hatua watendaji wake wanaosababisha kwa hoja za kiukaguzi pamoja na kutakiwa kuzijibu kwa wakati.

Katibu tawala mkoa  wa Njombe Catalina Revocati kwa niaba ya mkuu wa mkoa ametoa agizo hilo katika kikao cha baraza maalum la madiwani la kujadili hoja za CAG na kwamba pamoja na halmashauri hiyo kupata hati safi kwa miaka minne mfululizo lakini inapaswa kuzifanyia kazi hoja hizo huku mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri akielekeza kuwachukulia hatua watendaji wanaozalisha hoja za ukaguzi.


“Ninomba sana baraza litoe maelekezo ili mkurugenzi aweze kulifanyia kazi hasa swala la hoja kwenye ukusanyaji mapato katika leseni za biashara ili zisijitokeze tena wakati mwingine”alisema Catalina Revocati

“Watendaji wengi hawakaguliwi zinakuwepo hoja nyingi za wananchi ambazo wanahitaji majibu na hawapati majibu,oneni namna ya kuwafundisha na kuwakagua”alisema Ruth Msafiri

Baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo akiwemo Julius Salingwa,Roida Wandelage na Shaib Masasi wanasema pamoja na kuridhia kwa hoja hizo lakini wanataka hatua stahiki kuchukuliwa kwa watumishi ambao wamezalisha hoja hizo.

“Ukusanyaji wa hizi kodi imekuwaje watu wanaishi mpaka wanafika mahali  wanashindwa kulipa kodi mpaka wanatutengenezea hoja,tunaomba ukusanyaji ufanyike maana yake kututengeneza hoja kwenye halmashauri ni kutuharibia”alisema Roida Wandelage

Valentino Hongoli ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Njombe ametumia fursa hiyo kumuelekeza mkurugenzi mtendaji Juma Ally kuhakikisha anazijibu hoja zilizopo ndani ya uwezo wake haraka iwezekanavyo.

“Mkurugenzi jitahidi pamoja na timu yako kuhakikisha hoja hizi ambazo zimebaki kufungwa,zinasimamiwa ili kufungwa inavyotakiwa hasa zile ambazo zipo ndani ya uwezo wetu,zipo nyingine ambazo zipo nje ya uwezo wetu zinahitaji ufuatiliaji kwa mfano hoja za kuhusu tunahitaji kuajili watumishi wa kutosha inayotoa ajira ni serikali kuu” alisema Valentino Hongoli

Halmashauri ya wilaya ya Njombe imeendelea kupata hati safi kila mwaka kwa miaka minne mfululizo huku ikifanikiwa kuvuka lengo la makusanyo  ya ndani katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha.