52 wauawa katika maandamano ya kulaani mauaji ya mwanaharakati Ethiopia



Makumi ya watu wameuawa katika maandamano ya ghasia yaliyoibuka katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa baada ya muimbaji ya mwanaharakati mashuhuri kupigwa risasi na kuuawa.

Getachew Balcha, msemaji wa eneo la Oromiya amesema kwa akali watu 52 wakiwemo maafisa usalama wameuawa katika ghasia hizo, na kwamba majumba kadhaa ya kibiashara yameteketezwa moto katika maandamano hayo.

Kadhalika makumi ya watu wametiwa mbaroni akiwemo kiongozi wa upinzani kutoka kabila la Oromo, Bekele Gerba na mmliki mashuhuri wa vyombo vya habari na pia mwanaharakati wa kisiasa, Jawar Mohammed.

Maandamanamo hayo yaliibuka tangu Jumanne baada ya mwanamuziki na mwanaharakati mashuhuri nchini humo, Haacaaluu Hundeessaa kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana mjini Addis Ababa Jumatatu usiku.

Hundeessaa, 34,  ambaye ni kutoka kabila la Oromo alikuwa mashuhuri kwa nyimbo zake za kimapinduzi na kutetea haki. Mkuu wa Polisi mjini Addis Ababa, Geta Argaw amesema mwanaharakati huyo alikimbizwa hospitalini baada ya kupigwa risasi lakini alifariki kutokana na majeraha mabaya aliyoyapata.

Bado haijajulikani ni nani aliyehusika na mauaji hayo ambayo yamelaaniwa na maafisa wa serikali na raia ndani na nje ya nchi hiyo. Hata hivyo wafuasi wake wanasema mwanaharakati huyo aliuawa kutokana na nyimbo zake ambazo zilikuwa zinawahimiza watu wa kabila la Oromo waamke kutetea haki zao na wapambane na ukandamizaji.

Haacaaluu Hundeessaa anatazamiwa kuzikwa leo Alkhamis