https://monetag.com/?ref_id=TTIb Bei za ufuta Lindi zaendelea kuimarika | Muungwana BLOG

Bei za ufuta Lindi zaendelea kuimarika



Na Ahmad Mmow, Nachingwea.

Wakati msimu wa ununuzi wa ufuta kwa msimu wa 2020 ukielekea ukingoni. Bei za zao hilo zinaendelea kuimarika mkoani Lindi.

Ushahidi wa hilo unatokana na matokeo ya mnada wa saba kwa msimu wa 2020 katika chama kikuu cha ushirika cha RUNALI ambao umefanyika leo kijijini Mpiruka, wilaya ya Nachingwea.

Kwenye mnada huo ambao tani 2,734 na kilo 48 ambazo zipo katika maghala makuu ya Nachingwea, Liwale na Ruangwa ufuta huo umenunuliwa kwa  shilingi 1,895 ikiwa ni bei ya juu. Ambapo bei ya chini ni shilingi 1,860 kwa kila kilomoja.

Bei hizo nitofauti na bei za mnada wa sita uliofanyika juma lililopita wilayani Ruangwa. Kwani bei ya juu katika mnada huo wa sita ilikuwa shilingi 1,835. Wakati bei ya chini ilikuwa shilingi 1,820 kwakila kilo moja.

Ufuta huo uliouzwa na kununuliwa leo, katika ghala la Ruangwa ambao umenunuliwa na kampuni ya HS Impex Ltd lina tani 656 na kilo 78.

Katika maghala ya Nachingwea ambayo ufuta wake umenunuliwa na kampuni ya Mujibu Shamba Ltd yana tani 414 na kilo 10.

Wakati kampuni za Mujibu Shamba na HS Impex yakinunua katika maghala ya Nachingwea na Ruangwa. Kampuni za Afrisian, Nine Five Group, Digoziti  na RBST Ltd zimenunua tani 1,669 na kilo 960 zilizopo katika ghala la Liwale.

Wakati chama kikuu cha ushirika cha RUNALI kikifikisha minada saba kwa msimu huu wa 2020. Chama kikuu cha Lindi Mwambao kimefikisha minada nane. Vyama viwili vyote (Lindi Mwambao na RUNALI ) vyote vipo katika mkoa huu wa Lindi.