Chadema mchuano mkali wagombea,9 warejesha fomu za ubunge Njombe mjini


Na Amiri Kilagalila,Njombe
Joto la uchaguzi limezidi kupanda jimbo la Njombe mjini,ambapo wagombea 9 wa Chama cha Demokrasia na maendeleo Chadema mkoa wa Njombe wamefika ofisi za Chama hicho mkoa zilizopo halmashauri ya mji wa Njombe  na kurejesha fomu za kuomba ridhaa kwa Chama chao kugombea ubunge wa jimbo hilo.

Katibu  wa Chadema kanda ya nyasa Ndugu Emmanuel Masonga  ambaye amejitokeza tena kuchukuwa na kurejesha fomu ya ubunge huku akiwa na historia ya kuwa mgombea mwenza wa chama hicho jimbo la Njombe mjini 2015 aliyeangushwa na mgombea wa CCM Mh,Edward Mwalongo.Amesema pamoja na yaliyotokea kuanzia mwaka 2015,uongozi umeshindwa kutatua changamoto za wananchi wa jimbo la Njombe mjini.

“Pamoja na yale yaliyotokea yote,kipindi cha miaka mitano tumeona bado uongozi umeshindwa kutatua changamoto ambazo sisi ilikuwa ni ajenda zetu 2015,asilimia 80% ya wananchi wa jimbo la Njombe mjini ni wakulima hatujawahi kupata mbunge ambaye amejipambanua kuwatetea wakulima bungeni.sasa kwa mara nyingine tena nimekuja kuomba ridhaa ya chama change”amesema Emmanuel masonga

Mgombea mwingine ni mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Njombe baada ya kurejesha fomu amesema kilichomsukuma kugombea ni maono yake ya kupata kiongozi mwingine mwenye maono mapya.

“Njombe ina viongozi wapya waliotangulia lakini mimi nimeona iko sababu ya kupata kiongozi mwingine mwenye mtazamo mpya,mawazo mapya na fikra mpya ili tuweze kuitengeneza Njombe iliyo mpya,hatuwezi kuitengeneza Njombe mpya kwa mawazo ya ya zamani kwa hiyo ninaamini ninayo mawazo mapya mazuri ambayo yanaweza kuibadilisha Njombe yetu na ikawa moja kati ya maeneo bora Tanzania”alisema Rose Mayemba

Mgombea mwingine aliyerejesha fomu ni Mariet Joseph Mwalongoambaye amesema vipaumbele vyake ni Afya,elimu na maji na kuahidi endapo akipata nafasi ni lazima aweze kuvipigania

“Afya,Kilimo.Natamani kuona mabadiliko kwa kusaidiana na wananchi wenzangu,Njombe kila sehemu inatambulika kwa kasi kubwa ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi,nasimama kama kijana,mama kutafuta suluhisho” Mariet  Mwalongo akirejesha fomu ya kuomba ridhaa kugombea jimbo la Njombe mjini kupitia Chadema

Naye Siglada Mligo aliyekuwa diwani wa vita maalumu kata ya Njombe mjini amerejesha fomu huku akiahidi kwenda kutatau changamoto za wananchi kwa kupambana na kukamilisha miradi ambayo haijaweza kukamilika kwa miaka mingi.

“Mimi ni muumini wa matatizo ya wananchi namna gani tunaenda kutatua matatizo ya wananchi,tuna miradi mingi Njombe ya toka mwaka 2008 lakini Njombe ndio halmashauri pekee Tanzania inayoongoza kwa mapato kwanini miradi haiishi.hayo ndio mambo ambayo natamani nikipata ridhaa ya kuwa mbunge wa jimbo la Njombe mjini niweze kupambana na kuyapatia ufumbuzi”Alisema Siglada Mligo

Katibu wa Chadema jimbo la Njombe mjini George Sanga amesema walikuwa na mchakato wa kuchukuwa fomu tangu tarehe nne,lakini wanashukuru kuona wanachama tisa wamejitokeza na kurejesha fomu ndani ya muda huku wakiendelea kusubiri taratibu nyingine.

“Tulikuwa na mchakato wa kuchukuwa fomu tangu tarehe nne kama chama kilivyoelekeza,na tunashukuru wanachama 9 jumla wamefanikiwa kurudisha ndani ya muda kwa hiyo taratibu nyingine  zitaendelea ili tupate mtia nia mmoja wa kupeperusha bendera kwenye jimbo la Njombe mjini”alisema George Sanga

Jimbo la mjini ambalo limekuwa likiongozwa na Chama cha mapinduzi limeendelea kuvuta hamasa kwa vijana kutia nia katika vyama vyao ikiwemo CCM,CHADEMA,TLP,NCCR MAGEUZI na ACT ambapo kwa sasa baadhi ya vyama hivyo vimeanza kuonyesha  vugu vugu za kisiasa  ndani ya vyama vyao huku vikisubiri tume ya Taifa ya uchaguzi kuruhusu kampeni za  Rais,wabunge na madiwani.