Danny Trejo: Alikuwa mraibu wa dawa za kulevya, mwizi wa mabavu na sasa ni nyota wa filamu

Danny Trejo amepigwa risasi, akadungwa kisu, akakanyangwa kanyagwa, akaliwa na kuteswa … mara kadhaa.

'Con Air', 'Zombie Hunter' na '3-Headed Shark Attack' hizo ni filamu tatu tu ambazo aliishia kufa.

Kulingana na utafiti mmoja, mwanaume huyo, 76, ameshiriki filamu kama mhusika ambaye mwishoni anakufa mara kadhaa kuliko muhusika mwengine yeyote yule.

"Hilo linaonesha kwamba nimekuwa nikifanya kazi," anatania.

Na kama haukuwa unafahamu jina lake kabla ya kusoma taarifa hii, bila shaka utamtambua sura yake kwa kuwa ameshiriki mamia ya filamu, maonesho ya televisheni pamoja na gemu kadhaa.

Katika filamu anazoshiriki, nywele zake ni ndefu na mara nyingi huwa zinasokotwa hivi, kama anaigiza, kifua chake kilichochorwa tattoo huachwa wazi na pia huwa anabeba silaha.

"Nilipoanza kuwa maarufu, Kuna rafiki yangu mmoja aliniambia, 'Dunia nzima inaweza kufikiria wewe ni nyota wa filamu, lakini huwezi. Sitaki kuwa nyota wa filamu. Nataka kuwa mwigizaji mzuri tu."

Anatania kwamba alipoanza kuigiza filamu, kila wakati yeye alikuwa mhusika anayeishia gerezani, 'mfungwa namba moja', kwasababu ya muonekano wake na tabia zake vilevile.

Lakini kabla ya kuingia kwenye uigizaji, ukweli ni kwamba yeye alikuwa mfungwa.

Na sasa hivi mashabiki wake wengi watafahamu historia yake kupitia makala mapya ya 'The Rise of Danny Trejo.'

"Ni miujiza kwasababu hata sikutakiwa kuachiliwa huru miaka ya 1960," amezungumza na Radio 1 Newsbeat.

Bingwa wa bondia gerezani

Akikulia eneo la California, Trejo alikuwa anatumia dawa za kulevya akiwa kijana na muda wake mwingi wakati wa miaka ya 1960 alikuwa nje na ndani ya gereza kwa makosa mbalimbali ikiwemo wizi wa kimabavu.

Ndani ya gereza alikuwa anafahamika vyema, na akawa bingwa wa ndodi katika gereza kuu la San Quentin, gereza la zamani zaidi California.

Danny anakumbuka akishuhudia mfungwa mwenzake akidungwa kisu mgongoni.

"Alikuwa anatembea upande wa juu wa bustani, akijaribu kufikia kisu huku akiwa anakohoa damu, na kila mmoja akaanza kucheza. Ni eneo baya mno."

Danny pia amewahi kufungwa katika magereza mengine mawili - Soledad na Folsom - na anakubali kwamba kushiriki katika kuanda makala ya maisha ya ujana wake inamuuma sana.

"Nakumbuka nikiwa maambusu ya watoto Marekani na wakati huo nilifikiria kwamba sasa maisha yangu yameisha. Kwasababu hapo hapo ndani ya gereza utapata masomo pia.

"Nikajaribu kusema hapana, subiri kidogo. Mambo bado. Hapa ndio mwanzo unaanza."

Aliamua kubadili maisha yake kwa kuachana na dawa za kulevya.

Baada ya hapo akawa mshauri wa masuala ya dawa za kulevya na kuamua kutumia tajriba yake kusaidia wengine kabla ya kujiunga na tasnia ya filamu.

Na pia tangu alipoingia kwenye filamu amekuwa akijitahidi kuwa mwema kwasababu anafahamika fika kwamba umaarufu wake unaushawishi mkubwa na ana imani kwamba atahamasisha vijana wengine wengi mashabiki wake:

"Haijalishi unaanzia wapi, cha muhimu ni mwisho wako utakavyokuwa."

Katika makala, utamuona Danny akiingia gerezani na kushirikisha wafungwa tajriba yake mwenyewe. Anasema kila wakati anapokuwa huko, anavuta harufu ya 'uoga na wasiwasi'.

"Nilitoka gerezani na ninaota kwamba bado niko gerezani. Hilo linanifanya ghafla nina amka na linanikumbusha kwamba sistahili kwenda kinyume na sheria."

Kadiri muda unayokwenda amekuwa na ratiba yenye sughuli nyingi za kikazi na kuna baadhi ya mashabiki wake wanauliza atastaafu lini?