https://monetag.com/?ref_id=TTIb DC Chiwamba awaonya wapenda shari, bei ya ufuta si haba | Muungwana BLOG

DC Chiwamba awaonya wapenda shari, bei ya ufuta si haba

 Na Ahmad Mmow, Liwale.

Wakati pilikapilika za wanachama wa vyama siasa nchini zikiendelea kwakuviomba vyama vyao viwapitishe kuwa wagombea wa nafasi za udiwani, uwakilishi, ubunge na Urais.

Mkuu wa wilaya ya Liwale, Sarah Chiwamba amewaonya watu wanafikiria kufanya vurugu wakati wa uchaguzi watakiona cha moto.

 Chiwamba ametoa onyo hilo leo katika kijiji cha Nangano alipozungumza na wakulima waliokwenda kushuhudia mnada wa tano wa ufuta katika chama kikuu cha ushirika cha RUNALI uliofanyika kijijini hapo.

Chiwamba alisema uzoefu unaonesha kwamba katika vipindi vya chaguzi baadhi ya wanasiasa ambao wanashindwa kuwashawishi wananchi waviamini vyama na wagombea wao wanawatumia vijana wafanye vurugu.

 Chiwamba alionya kuwa tabia hiyo haikubaliki na hakuna mwenye haki ya kuwatumia watu wengine kama mtaji wa kufikia malengo yao yakisiasa kwakuwashawishi wafanye vitendo vya uvunjifu wa amani.

 Alisema yeye kama mkuu wa wilaya hiyo hatavumilia hali hiyo itakapotokea. Kwahiyo atashughulika na watu hao kwa mujibu wa sheria na kwamamlaka aliyonayo.

 '' Kabla ya kufikiria kufanya vurugu jifikirie mwenyewe na wazazi wako. Atakaye thubutu kufanya vurugu nitakulanae sahani moja,'' alionya Chiwamba.

Mbali ya hilo, Chiwamba aliwakumbusha wakulima wasisahau kulima mazao ya chakula. Kwani kuzalisha mazao ya biashara bila mazao ya  chakula kutasababisha uhaba wa chakula wilayani humo.

 Mkuu huyo wa wilaya ya Liwale alibainisha kwamba licha ya ardhi ya wilaya hiyo kuwa na rutuba nzuri kwa mazao ya biashara kama korosho, ufuta na mbaazi.

Lakini pia inasitawisha mazao ya aina mbalimbali ya chakula. Katika hatua nyingine mwakilishi huyo wa Rais katika eneo la utawala la wilaya ya Liwale amewaasa wananchi waliopo kwenye mpango wa bima ya afya watakao nyanyaswa katika vituo vya kutolea huduma za afya wawasiliane nae moja kwa moja.

Huku akiwatajia namba za laini ya simu yake ya mkononi. Katika mnada wa leo tani 3050 na kilo 132 ambazo zilikuwa katika maghala makuu ya chama cha RUNALI yaliyo Ruangwa, Nachingwea na Liwale ulinunuliwa kwa bei ya juu ya shilingi 1,867 na bei ya chini ni shilingi 1,863.

Kampuni zilizofanikiwa kushinda mnada na kupewa haki ya kununua ufutao huo ni Inishieta, RBST, Tanzania& China, HS Impex na Hy carry.