Magaidi 5 wa al-Shabaab waangamizwa kusini mwa Somalia


Jeshi la Kitaifa la Somalia limetangaza habari ya kuangamiza wanachama watano wa kundi la kigaidi la al-Shabaab huko kusini magharibi mwa nchi.

Ibrahim Mohamed Nour, Gavana wa mji wa Awdinle amethibitisha habari hizo Jumatatu na kuongeza kuwa, magaidi hao waliuawa katika makabiliano na wanajeshi wa serikali katika eneo la kusini la Bay, na kwamba wengine sita wamejeruhiwa.

Nour ameongeza kuwa, "wanajeshi wetu wamefanikiwa kutibua njama za maadui za kutaka kuteka na kudhibiti kambi ya kijeshi katika jimbo la kusini magharibi mwa nchi."

Gavana huyo amesema wameanzisha msako wa kuwatafuta wanachama wengine wa genge hilo waliotoroka baada ya kukabiliwa vikali na wanajeshi wa serikali.

Haya yanajiri siku mbili baada ya watu watano kuuawa na wengine 10 kujeruhiwa katika shambulizi la bomu lililofanywa na magaidi wa al-Shabaab katika mji wa Baidoa katika eneo hilo hilo la Bay.

Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe karibu miaka 30 iliyopita na magaidi wakufurishaji wa al-Shabaab walianzisha hujuma dhidi ya nchi hiyo mwaka 2008.