Poland yakabiliwa kinyang'anyiro kikali cha duru ya pili ya uchaguzi wa rais

Wapiga kura nchini Poland kesho wataamua katika kinyang'anyiro kikali cha duru ya pili ya uchaguzi kati ya Rais wa sasa Andrzej Duda na mpinzani wake wa kiliberali anayeelemea upande wa Umoja wa Ulaya, Meya wa Warsaw Rafal Trzaskowski.

Uchunguzi wa karibuni wa maoni unaonyesha kivumbi kikali ambacho huenda kikaamuliwa na tofauti ndogo sana ya wapiga kura katika taifa hilo la Umoja wa Ulaya lenye idadi ya watu milioni 38.

Kama Duda atashinda, yeye na chama cha siasa za mrengo wa kulia cha Sheria na Haki ambacho kinamuunga mkono atashikilia karibu vyombo vyote vya dola, hadi labda uchaguzi ujao wa bunge wa 2023.

Chama chake cha Sheria na Haki kimeleta mgawanyiko katika jamii kwa kuyatenga makundi ya walio wachache na pia kukosolewa na baadhi ya viongozi wa Umoja wa Ulaya kwa sababu ya sheria zinazokipa chama hicho nguvu mpya dhidi ya mfumo wa sheria nchini humo.

Ushindi kwa Trzaskowski, wa chama cha upinzani, cha Civic Platform, huenda kikampa kura ya turufu kupinga sheria zilizopitishwa na chama tawala.