Sudan yafanyia mabadiliko sheria zake na kuwaruhusu raia kunywa pombe


Wizara ya haki na sheria nchini Sudani imetangaza mabadiliko ya kukomesha hukumu ya kifo kwa sababu ya kuasi dini, kupiga marufuku ukeketaji na ruhusa kwa Wakristo kunywa pombe.

Wanawake pia hawatahitajika kupata ruhusa kutoka kwa wanaume au walezi kusafiri na watoto wao.

Vinywaji vya ulevi vilipigwa marufuku nchini Sudan wakati Rais Ja'afar Nimeiri alipotangza sheria ya kiislamu mwaka 1983.

Sheria hiyo iliendelea kufanya kazi wakati wa utawala wa Rais Omar al-Bashir ambaye aliondolewa madarakani mwaka 2019.

Waziri wa sheria Nasreldin Abdelbari amesema kuwa madiliko hayo kutekeleza maazimio ya kikatiba ya mwaka 2019 kwa kuzingatia ''uharaka wa kuhakikisha kuwa kuna uhuru na utawala wa sheria bila kuwepo kwa ubaguzi.''

Vuguvugu la kiislamu nchini humo imeanzisha kampeni ya vyombo vya habari dhidi ya mabadiliko hayo wakiyaita ''vita dhidi ya maadili na ukaidi dhidi ya dini na utambulisho nchini humo''.

Katika hatua nyingine , mamlaka katika jimbo la Kaskazini mwa Darfur limetangaza hali ya dharura ya siku 15 mjini Kutum baada ya kutokea mapigano kati ya vikosi vya usalama na raia.

Mashuhuda walisema polisi walitumia gesi ya kutoa machozi tarehe 12 mwezi Julai kuwatawanya ''watu waliokuwa wakikusanyika kwa amani '' mjini Kutum lakini mamlaka zimesema kuwa watu waliwashambulia polisi na kuchoma moto magari yao.

Karibu watu 11 walijeruhiwa wakati wa mapambano hayo. Waandamanaji mjini Kutum wamekuwa wakitaka kuondoshwa kwa wanamgambo wenye silaha.