Uholanzi kuishtaki Urusi katika mahakama ya Ulaya kwa kuidungua ndege ya Malaysia

Uholanzi imesema itaishtaki Urusi katika mahakama ya Ulaya kuhusu haki za binadamu ya ECHR kwa hatua yake ya kuidungua ndege ya shirika la ndege la Malaysia mwaka 2014.

Jamaa wa wahanga 65 wa Uholanzi waliofariki kwenye ajali ya ndege waliwasilisha malalamiko yao kwenye mahakama hiyo yenye makao yake mjini Strasbourg, wakiitaka Urusi kubeba dhamana ya tukio hilo ambamo watu wote waliokuwa kwenye hiyo waliuawa.

Uholanzi na Australia zimesema zinaibebesha jukumu Urusi kwa kuidungua ndege hiyo, iliyokuwa safarini kuelekea Kuala Lumpur kutoka Amsterdam.

Waziri wa mambo ya nje wa Uholanzi Stef Blok amesema upatikanaji wa haki kwa wahanga 298 wa ndege hiyo iliyokuwa na nambari za safari MH17, utaendelea kuwa kipaumbele cha juu kabisaa cha serikali yake.