Wabosnia wakumbuka miaka 25 ya mauaji ya Srebrenica

Raia wa Bosnia wamefanya kumbukumbu ya mauaji ya halaiki ya Waislamu 8,000 ya Srebrenica ikiwa miaka 25 tangu kufanyika kwa mauaji hayo yaliyoushtua ulimwengu na yamekuwa ndio udhalimu pekee mkubwa uliofanyika Ulaya tangu Vita vya Pili Vikuu vya Dunia.

Familia zinazoomboleza zilisimama mbele ya majeneza tisa ya wahanga wapya waliotambuliwa yaliyokuwa yamefunikwa kwa kitambaa cha kijani.

Wahanga hao wapya wamezikwa katika eneo la makaburi lililo na umbo la ua sehemu iliyo na makaburi ya wahanga wengine 6,643. Karibu wahanga 1,000 wa mauaji hayo ya halaiki katika mji huo wa mashariki yaliyotokea wakati wa vita vya Bosnia vya kati ya mwaka 1992-1995 bado hawajulikani walipo.

Viongozi wa dunia wamehutubia sherehe hizo za maadhimisho kwa njia ya video kwani hawakuweza kuhudhuria kutokana na janga la virusi vya corona.

Wakati wa vita vya Bosnia, wanajeshi wa Waserbia waBosnia waliwafukuza watu ambao si raia wa Serbia kutoka maeneo hayo.

Waislamu waliokuwa wanatoroka walijificha katika miji ya mashariki ukiwemo mji wa Srebrenica ambao ulikuwa ni mmoja wa miji iliyokuwa imedaiwa kuwa maeneo salama yaliyotengwa na Umoja wa Mataifa.