WHO: Watu wengine 230,000 waambukizwa corona ndani ya saa 24


Shirika la Afya Duniani WHO, limerekodi idadi mpya ya juu zaidi, ya maambukizi mapya ya virusi vya corona, ya watu 230,000 ndani ya saa 24 zilizopita.

Shirika hilo limesema jana Jumapili, kwamba Marekani imerekodi zaidi ya maambukizi mapya 66,000, na hivyo kuongoza kwa mara nyingine miongoni mwa nchi ambazo zimeathiriwa zaidi. Jimbo la Florida pekee likiwa limerekodi maambukizi mapya 15,000.

Katika siku tatu zilizopita, WHO imerekodi maambukizi mengi. Mnamo Ijumaa zaidi ya maambukizi 228,000 yalirekodiwa ulimwenguni kote ndani ya saa 24.

 Kwa jumla, watu milioni 12.5 ulimwenguni kote wamethibitishwa kuambukizwa, na zaidi ya watu 561,000 wamefariki kutokana na ugonjwa wa COVID-19.

 Mexico imekuwa taifa la nne lenye idadi kubwa ya vifo baada ya kurekodi jumla ya vifo 35,006, na hivyo kuipita Italia ambayo ilikuwa na jumla ya vifo 34,954.