Balozi Seif Iddi: Ushirikiano wa karibu wa serikali zote mbili umeonyesha mwanga mzuri uliolifanya Taifa la Tanzania kuingia kwenye Uchumi wa kati

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ushirikiano wa karibu unaoendelea kuimarika kati ya Wizara zinazosimamia Sekta ya Nishati na Madini za Serikali zote mbili ile ya SMT na SMZ umeonyesha mwanga mzuri uliolifanya Taifa la Tanzania kuingia kwenye Uchumi wa kati kwa kujiamini.


Alisema kasi kubwa ya uwekezaji kwenye Sekta ya Viwanda, Biashara, Utalii na hata Miji Mipya ya Kisasa inayojengwa katika maeneo mbali mbali Nchini Bara na Zanzibar inahitaji kupata nguvu kubwa ya Nishati hiyo ya Umeme.


Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo kwenye Makaazi yake yaliyopo Mtaa wa Farahani Jijini Dodoma wakati akizungumza na Waziri anayesimamia Wizara ya Nishati na Madini wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Medard Kalemani aliyefika kubadilishana nae mawazo.


Alisema Taifa limeshadidia kasi ya ujenzi wa Miundombinu katika Sekta ya Viwanda Bara na Zanzibar ambayo lazima wahusika wa kazi hiyo wahakikishe wanasimamia jukumu lao ili lile kundi la Wasomi linalomaliza masomo yao liingie kwenye ajira katika eneo hilo muhimu.


Alifahamisha kwamba Wapo Vijana wengi wanaomaliza Masomo yao ya Vyuo Vikuu pamoja na  Elimu ya Sekondari wanaohitaji Ajira ili kuendesha Maisha yao ambapo njia pekee kwa sasa ya kukabiliana na tatizo la ajira ni kuimarika kwa Sekta ya Viwanda.


Balozi Seif aliishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kupitia Wizara ya Nishati pamoja na Shirika la Umeme Tanzania {TANESCO} kwa uamuzi wake wa kusamehe Madeni yaliyokuwa yakilidai Shirika la Umeme Zanzibar {ZECO} kwa kipindi kirefu.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuomba Uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini na ule ya Shirika la Umeme Tanzania {TANESCO} kuendelea kulipatia msaada Shirika la Umeme Zanzibar { ZECO}ili kuona huduma za nishati ya Umeme zinamfikia kila muhitaji.


Mapema Waziri wa Nishati na Madini  wa Serikali ya Jamuhuri yaMuungano wa Tanzania Dr. Medard Kalemani alisema Wizara anayoisimamia kupitia Shirika la Umeme Tanzania wakati wote inahakikisha kuona kwamba huduma ya Umeme inapatikana wakati wote katika maeneo yote Tanzania Bara na Zanzibar.


Dr. Kalemani alisema huduma ya umeme kwa sasa ni suala la lazima katika mazingira halisi ya kimaisha ya Mwanaadamu jambo ambalo halina mbadala katika upatikanaji wake.


Waziri huyo wa Nishati na Madini wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Zanzibar inayopata Huduma za Umeme katika vianzio vilivyopo Tanzania Bara itaendelea kupata huduma hiyo kwa wakati wote.


Alisema pale inapotokea kufanyika kwa huduma za kiufundi  ikiwemo kubadilisha kwa zana na  vifaa vipya utaratibu wa kutolewa Taarifa mapema huzingatiwa ili kujiepuka  na usumbufu unaoweza kuleta athari.


 


 

Post a Comment

0 Comments