Mji wa Nagasaki waadhimisha miaka 75 ya shambulizi la nyuklia

Mji wa Nagasaki nchini Japan leo umeadhimisha miaka 75 tangu shambulizi baya kabisa la nyuklia lililofanywa na Marekani mwaka 1945 na kuwauwa zaidi ya watu 74,000.

Mji wa Nagasaki uliharibiwa kabisa kwa kishindo cha bomu la Atomiki siku tatu baada ya shambulizi kama hilo kufanywa dhidi ya mji mwingine wa Japan wa Hirishoma ambako watu 140,000 walikufa.

Katika maadhimisho ya leo, wahanga, ndugu wa waliokufa na wawakilishi wa kimataifa walishiriki halfa ya kumbukumbu iliyofanyika mjini Nagasaki ambayo kabla ilitanguliwa na ibada ya kidini. Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe amerejea ahadi yake ya kuongoza juhudi za kimataifa za kukomesha utengenezaji na matumizi ya silaha za nyuklia.

Kwa upande wake, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya kuwa matumizi ya silaha za nyuklia ni hatari na kutoa wito wa kuimarisha juhudi za kutokomeza shehena ya silaha za nyuklia duniani.