https://monetag.com/?ref_id=TTIb Mkandarasi barabara ya Ludewa amchefua Waziri Kamwelwe “Sitarajii wampe tena nyongeza ya muda” | Muungwana BLOG

Mkandarasi barabara ya Ludewa amchefua Waziri Kamwelwe “Sitarajii wampe tena nyongeza ya muda”


Na Amiri Kilagalila,Njombe

Waziri wa ujenzi Uchukuzi na mawasiliano Eng,Isack Kamwelwe amemuagiza mkandarasi anayejenga mradi wa barabara kipande cha Kilomita 50 kutoka Lusitu kwenda Mawengi ambayo ni sehemu ya Itoni-Ludewa-Manda wilayani Ludewa Mkoani Njombe kwa kiwango cha zege,kuweka mipango vizuri ya ujenzi ili kuhakikisha bara bara hiyo inakamilika kwa kuwa mradi huo umeanza muda mrefu na kushindwa kukamilika mpaka sasa.

Waziri Kamwelwe ametoa agizo hilo alipotembelea  na kukagua maendeleo ya barabara hiyo mkoani Njombe na kushindwa kuridhika kutokana na kuchukuwa muda mrefu huku ikiwa bado haijakamilika.

“Kazi hii ilianza mwezi Disemba mwaka 2016,kwa hiyo 2017 imeisha, 18 imeisha, 19 imeisha na tuko sasa 20 mwezi wa nane.Mkandarasi huyu anaonekana ni mgeni pamoja na kwamba wakati wa manunuzi alionekana ana uwezo mkubwa,kazi anayofanya ni nzuri lakini naona alishindwa kufanya mipango”alisema Waziri Kamwelwe

Aidha Waziri Kamwelwe amesema mkandarasi anayejenga bara bara hiyo ameshindwa pia kwenda na wakati kutokana na kuwa na mitambo michache hivyo hatarajii kuona anapewa nyongeza ya muda.

“Mitambo aliyoleta imekuwa ni michache hasa ya kubeba udongo ndio maana amechukuwa muda mrefu,mradi huu ulikuwa na wa miezi 28 wakamuongezea ikafika miezi 46 ambayo inaisha mwezi wa 10 mwaka huu,mimi sitarajii wampe tena nyongeza ya muda na kama mhandisi mshauri atataka ziongezeka fedha za kumlipa basi serikali haita toa hilo ndio agizo langu,mkandarasi kwasababu yeye ndio aliyechelewesha tutakuwa tunamega hela yake halafu tunalipa mshahara wa msimamizi” aliongeza Kamwelwe

Vile vile ameagiza wakala wa barabara Tanzania TANROADS kupeleka wataalam waweze kuongeza bidii kusimamia kazi hiyo kwa kuwa bara bara hiyo itatumika kubeba mzigo mkubwa pindi itakapoanza zoezi la uchimbaji wa madini ya Chuma na makaa yam awe hivyo ni lazima asimamiwe ili kazi hiyo iweze kukamilika mapema mwezi Octoba.

Aidha kwa upande wake meneja wa TANROADS mkoa wa Njombe mhandisi Yusuph Mazana,amesema mradi huo uliopo chini ya mkandarasi Cheon Kwang Engenginearing & Construction Copamany ya Korea Kusini,unaotarajia kujengwa kwa ghalama ya shilingi Bilioni 179.17 za fedha za serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100%, mpaka sasa umefikia asilimia 45.35%

“Utekelezaji wa mradi huu ambao unatakiwa ukamilike tarehe 30 Octoba,2020 mpaka sasa umefikia asilimia 45.35, na mpaka sasa mikakati ya kupunguza kuchelewa kwa kazi,mkandarasi ameleta wataalam makini sasa hivi,mkandarasi ameweza kuleta vifaa vyote vinavyotakiwa na ameongeza kasi ya ujenzi kwa kufanya kazi kwa muda mrefu”alisema Mazana

 

Post a Comment

0 Comments