Niyonzima atua Azam FC

Klabu ya Azam FC imekamilisha usajili wa kiungo mkabaji wa kimataifa wa Rwanda, Ally Niyonzima, kwa mkataba wa miaka miwili.

Niyonzima aliyekuwa akicheza Rayon Sports ya Rwanda, usajili wake ni sehemu ya mapendekezo ya benchi la ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu, Mromania Aristica Cioaba.

Kiungo huyo nyota mwenye umbo kubwa, amesaini mkataba mbele ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’.

Niyonzima, ambaye yumo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Rwanda, ‘Amavubi’, anakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa Azam FC kwa ajili ya msimu ujao baada ya kiungo mwingine, mzawa Awesu Awesu kutoka Kagera Sugar ya Bukoba.