Serikali kutoa ajira mpya za walimu shule za sekondari na msingi

Serikali imesema itatoa ajira mpya 12,000  za walimu wa shule za sekondari na msingi pale taratibu za kuajiri zitakapo kamilika.

Kauli hiyo imebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo wakati alipokuwa akitoa mrejesho kwa wa  mafanikio kwa wananchi kwa yaliyotekelezwa na serikali ndani ya miaka mitano katika sekta ya  Elimu (ELIMU DAY –TAMISEMI) leo Jijini Dodoma.


Aidha Mhe. Jafo amesema kuwa  zaidi ya walimu  18,000 wameajiriwa na kupelekwa Shule za Msingi na Sekondari na ajira mpya 12,000 ziko katika taratibu za mwisho kuweza kukamilika kutokana na maelekezo yake Rais John Magufuli bado taratibu zake zinaendelea.

Mhe.Jafo amesema kuwa  changamoto ninyingi na haziwezi kuisha ila  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli  amaelekeza kuongeza ajira za walimu hivyo taratibu zikikamilika watanzania wapate kuchangamkia fursa hiyo.

Mhe. Jafo amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana kwa miaka mitano katika Sekta ya Elimu ya Msingi na Sekondari  ndani ya  kipindi cha muda mfupi, kiasi cha Sh.Trilioni 1.09 zimetumika kutoa elimu bila malipo kwa watanzania.


“Zaidi ya Sh.Bilioni 502 zimetolewa kwa ajili ya elimu ya Shule za Msingi na Sh.Bilioni 593.9 zimetumika katika shule za sekondari, jambo ambalo limesaidia watoto wa watanzania wenye kipato cha chini  kupata elimu”ameeleza Mhe. Jafo.

Pia Mhe. Jafo serikali imetoa  Sh.Bilioni 501 kwa ajili ya kuboresha miundombinu mbalimbali na hadi kufikia mwezi Juni 2020 ujenzi wa shule mpya za Msingi 905 zilikuwa zimekamilika na kufanya  idadi ya shule za Msingi kutoka 16,899  hadi 17,804 .

Kwa kuongezea Mhe. Jafo amesema kuwa  vyumba vya madarasa 17,215 vimejengwa na kuongezeka kutoka vyumba 108,504 mwaka 2016 hadi 125,719 mwaka 2020, sawa na ongezeko la asilimia 13.7 ambapo ujenzi wa vyumba 3,049 unaendelea na ukikamilika idadi ya vyumba vya madarasa kwa shule za Msingi itafikia 128,768.

Katika hatua nyingine Mhe. Jafo amesema kuwa  serikali imejenga shule mpya za Sekondari 228 na hivyo kutoka  shule 4,708 mwaka 2016 hadi 5,330 mwaka 2020.

Naye  Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Mhandisi Joseph Nyamhanga, amesema uwekezaji na maboresho yaliyofanyika katika sekta ya elimu kwa shule za msingi na sekondari umesaidia kuongeza kiwango cha ufaulu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi  kwa asilimia 81.50 mwaka 2019.

Huku  Naibu Katibu Mkuu, TAMISEMI  anayeshughulikia Elimu, Gerald Mweli, amesema Mpango wa Elimu bila malipo  ulianzishwa baada ya kufanyika utafiti na kugundua idadi kubwa ya watoto wakitanzania walikuwa hawaendi shule kutokana na wazazi na walezi kukosa ada.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa wanafunzi wote kuhakikisha wanatunza miundombinu ya shule ili serikali ipate nguvu zaidi  kwa kuendelea kuboresha katika mambo mengine ili kuimarisha uchumi wa kati.