Barua yenye sumu ilitumwa kwa Trump katika White House


Kifurushi kilichokuwa na sumu ya ricin ambacho kilikuwa na awani ya rais wa Marekani Donald Trump kimezuiwa kabla ya kufika katika White House, maafisa wameviambia vyombo vya habari vya Marekani.


Barua hiyo iligunduliwa katika kitengo cha ukaguzi wa vifurushi vya barua katika Ikulu ya White House mapema wiki hii , wanasema maafisa.


Walisema kuwa sumu hiyo iliyopatikana ndani ya bahasha ilitambuliwa kama ricin, sumu ambayo kwa kawaida hupatikana katika maharagwe.


Utawala wa Trump haujasema lolote kuhusiana na taarifa hiyo.


FBI pamoja na huduma za upepelezi wa siri wanachunguza kubaini ni wapi kifurushi hicho kilitoka na iwapo vifurushi vingine vya aina hiyo vilitumwakupitia mifumo ya posta ya Marekani.


"Wakati huu hakuna tisho linalofahamika la usalama kwa umma ," FBI iliiambia televisheni ya CNN katika taarifa yake Jumamosi. Afisa mmoja ameliambia gazeti la New York Times nchini humo kuwa wachunguzi wanaamini kifurushi hicho kilitumwa kutoka Canada. taarifa zinasema uwepo wa sumu ya ricin ulithibitishwa baada ya vipimo vya FBI.


Polisi ya Canada-The Royal Canadian Mounted Police (RCMP) ilisema Jumamosi kuwa inashirikiana kwa pamoja na FBI kuchuguza barua "inayoshukiwa iliyotumwa katika ikulu ya White House".


Ricin hutengenezwa kwa kusindikwa kwa maharage ya castor . Ni sumu inayoua ambayo kama ikimezwa, kuivuta wakati wa kupumua au kuchomwa sindano yake , inaweza kusababisha kizunguzungu, kutapika, kuvuja damu ndani ya mwili na kusimamisha utendaji wa viungo vya ndani ya mwili.


Iwapo mtu atatumia sumu ya ricin, kifo chake kinaweza kutokea katika kipindi cha saa 36 na 72, kulingana na kiwango cha dozi iliyoingia mwilini mwake, kwa mujibu wa Kituo cha Marekani cha kudhibiti na kuzuwia magonjwa (CDC).


CDC kinasema sumu hiyo-ambayo imekwishawahi kutumiwa katika njama za ugaidi-inaweza kutengenezwa kuwa silaha katika muundo wa poda, au mvuke.


White House na majengo mengine ya serikali kuu ya Marekani yaliwahi kulengwa kwa kutumia sumu ya aina hiyo miaka iliyopita.


Mwaka 2014, mwanaume mmoja wa Mississippi alihukumiwa kifungo cha miaka 25 gerezani kwa kutuma barua iliyokuwa na poda ya sumu ya ricin kwa rais Barack Obama na maafisa wengine:https://www.bbc.com/swahili/habari/2014/07/140717_ricin_obama


Miaka minne baadaye, mwaka 2018, mwanajeshi wa zamani wa kikosi cha majini cha Marekani alishitakiwa kwa kutuma sumu hiyo katika ofisi za makao makuu ya jeshi la Marekani-Pentagon na ikulu ya White House.

Post a Comment

0 Comments