https://monetag.com/?ref_id=TTIb Ditopile: Magufuli karahisisha maisha ya wafanyabiashara wadogo kupitia vitambulisho vya mjasiriamali | Muungwana BLOG

Ditopile: Magufuli karahisisha maisha ya wafanyabiashara wadogo kupitia vitambulisho vya mjasiriamali

KAMPENI za Udiwani Kata ya Madukani zimezinduliwa rasmi na Mgombea Ubunge wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile ambaye amemnadi na kumuombea kura mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli, mgombea Ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde na mgombea Udiwani wa kata hiyo, Prof Devis Mwamfupe.


Akizungumza katika kampeni hizo, Ditopile amesema kata ya Madukani ni miongoni mwa kata zilizonufaika na uongozi wa Dk Magufuli kutokana na kutoa fursa kubwa kwa wafanyabiashara kufanya biashara kwa Uhuru bila kubughudhiwa.

Amesema Madukani ni kata ambayo asilimia kubwa ya wakazi wake ni wafanyabiashara hivyo kuwaomba Oktoba 28 kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Rais Magufuli ili azidi kuwatumikia na kuweka mazingira mazuri na bora kwa wafanyabiashara ambao kwa miaka mitano ya uongozi wake wamenufaika na vitambulisho vya mjasiriamali.

" Wafanyabiashara kwa miaka minne tumenufaika kwa kiasi kikubwa na hivi vitambulisho vya wajasiriamali ambavyo vilitolewa kwa upendo mkubwa na Rais Magufuli kwa sababu ya kujali wananchi wake hasa wale wanyonge, ameishi ahadi yake aliyoitoa mwaka 2015 ya kuwatumikia wanyonge kweli tunaona namna anavyotujali.

Anapokuja mtu anawaambia hivi vitambulisho mnaibiwa inabidi mumpuuze na kumkataa, mwanzoni Mama muuza mboga alikua analipia Sh 500 ya ushuru ambayo kwa miezi 10 tu Sh 140,000 leo Magufuli amesema hapana hawa watu watalipa 20,000 kwa mwaka mzima.

Niwambie tu hivi vitambulisho vimepunguza mapato sana lakini Dk Magufuli yeye hilo hajaliangalia kaangalia wepesi wa wananchi wake wanyonge kufanya kazi na kujipatia riziki, lakini siyo hivyo tu akasema msiguswe na mfanye biashara popote pale, wapi tutapata kiongozi mwenye kujali wananchi wake hivyo," " Amesema Ditopile.

Amesema vijana wa Bodaboda nao wamenufaika na serikali ya Dk Magufuli kwani siku hizi hakuna kukamatwa hovyo jambo ambalo pia limerahisisha ufanyaji kazi wa kundi hilo kubwa la vijana waliojiri wenyewe.

Ditopile ameomba watanzania kuwapuuza wapinzani kwani wamekua wakipinga kila kitu hata vile vinavyohusu maendeleo ya wananchi.

" Wenzetu wanapinga kila kitu lakini kibaya hawana mbadala, huyo mmoja anaponda maendeleo yaliyofanyika kwenye sekta ya Afya lakini alipopata ajali yake alipatiwa huduma ya kwanza kwenye Hospitali yetu ya Mkoa, wanaponda ununuzi wa Ndege zetu ila wote ni mashahidi wao wenyewe ni watumiaji wa ndege hizo, wanalalamikia miundombinu ya barabara na bado wanapita kwenye hizo hizo barabara zilizojengwa na Magufuli, tuwaepuke matapeli wa kisiasa hao," Amesema Ditopile.

Amewasihi wananchi wa Madukani kutofanya makosa kumchagua Diwani wa upinzani na badala yake wamchague Prof Mwamfupe ubunge wampe Mavunde na kura za Urais wakapige kwa kishindo kwa Dk Magufuli ili kwa pamoja watengeneze mafiga matatu ya kuwatumikia.

Kwa upande wake mgombea Udiwani wa Madukani, Prof Devis Mwamfupe amewaomba wananchi wa kata hiyo kumchagua huku akiwaahidi utendaji kata wenye kuwasikiliza na kuwaelewa zaidi wananchi kuliko yeye kueleweka kwao.

 

Post a Comment

0 Comments