Kiongozi wa upinzani wa Belarus ataka jamii ya kimataifa kuchukua hatua kali kufuatia visa vya unyanyasaji

 


Kiongozi wa upinzani wa Belarus Svetlana Tikhanovskaya ameitolea wito jamii ya kimataifa kuchukua hatua kali dhidi ya Belarus kufuatia visa vya unyanyasaji nchini mwake, wakati akihutubia baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa.

Tikhanovskaya, ambaye amekimbilia nchi jirani ya Lithuania ametoa wito huo kwa njia ya video wakati wa kikao cha kujadili kadhia ya Belarus.

Kiongozi huyo wa upinzani amesema hali nchini mwake inahitaji uangalizi wa haraka wa kimataifa.Kikao cha kujadili kadhia ya Belarus kiliitishwa na Umoja wa Ulaya ili kuangazia ukiukaji wa haki za binadamu nchini Belarus hasa ukandamizaji dhidi ya waandamanaji.

Maandamano makubwa yaliibuka nchini humo baada ya rais Alexander Lukashenko ambaye ameitawala Belarus kwa miaka 26 kutangazwa mshindi kwa asilimia 80 ya kura katika uchaguzi wa Agosti 9.

Lukashenko ambaye jana Alhamisi alionya juu ya uwezekano wa vita na baadhi ya nchi jirani amekataa kujiuzulu na ameigeukia Urusi kwa msaada.


Post a Comment

0 Comments