Israel yanyooshewa kidole mauaji ya mwanasayansi wa Iran


Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Javad Zarif amesema kuna ushahidi unaoashiria uhusika wa Israel katika mauaji ya Mohsen Fakhrizade lakini haikuwa wazi ni nani hasa aliyefanya shambulizi hilo.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Iran imethibitisha kifo cha mwanasayansi mwandamizi wa nyuklia nchini humo Mohsen Fakhrizadeh. Fakhrizadeh alifyatuliwa risasi na kujeruhiwa na "magaidi" wakati akiwa kwenye gari yake katika eneo la Ab-Sard mashariki mwa Tehran na baadae kufariki dunia.

Mamlaka za eneo hilo zilithibitisha kifo chake masaa kadhaa na kusema kwama baadhi ya washambuliaji pia waliuawa. Fakhrizade, 63, alikuwa mwanachama wa kikosi cha walinzi wa kimapinduzi cha Iran na alikuwa mtaalamu wa uzalishaji wa makombora. Kulingana na shirika la habari la Fars, hii ndio sababu shirika la kijasusi la Israel kwa muda mrefu lilitaka kummaliza mwanasayansi huyo.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Javad Zarif amesema kuna ushahidi unaoashiria uhusika wa Israel katika mauaji hayo, lakini haikuwa wazi ni nani hasa aliyefanya shambulizi hilo.

Uthibitisho wa mauaji hayo unatolewa katikati ya wasiwasi mpya kuhusu kiwango cha urutubishaji wa madini ya urani ambayo taifa hilo inayazalisha.

Mwaka 2015, makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na mataifa makubwa yaliweka ukomo wa uzalishaji wa madini hayo ya urani, lakini rais Donald Trump alijiondoa miaka mitatu baadae. Rais mteule Joe Biden ameahidi kuirejesha Marekani kwenye makubaliano hayo, ingawa wachambuzi wanasema atakabiliwa na changamoto kubwa kulifanikisha lengo hilo.

Mapema Ijumaa hii, msemaji wa shirika la nguvu za Atomiki la Iran, AEOI Behrus Kamalwandi alisababisha sintofahamu kwa kuzikana ripoti za kifo cha mwanasayansi huyo akisema "wanasayansi wetu wote wako salama". Hali hiyo ya sintofahamu iliibuka kwa kuwa Fakhrizadeh alikwishaondoka AEOI na amekuwa akifanya kazi kwenye idara ya utafiti na uendelezwaji wa teknolojia katika wizara ya mambo ya kigeni.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa mwito wa kujizuia baada ya mauaji hayo. Msemaji wa Umoja huo Farhan Haq ameliambia shirika la habari la DPA kwamba " Tumezipata taarifa kwamba mwanasayansi wa nyuklia wa Iran ameuawa karibu na Tehran leo". "Tunaomba kujizuia na kujiepusha na hatua ambazo zinaweza kusababisha kusambaa kwa wasiwasi wa kikanda".

Mwanasanyansi huyo kwa muda mrefu amekuwa akichukuliwa na mataifa ya magharibi kama kiongozi wa programu ya siri ya bomu la nyuklia. Mauaji hayo huenda yakaibua mzozo mpya kati ya Iran na wapinzani wake, katika wiki za mwisho za utawala wa serikali ya rais Donald Trump wa Marekani, lakini pia kuleta ugumu katika juhudi zozote zinazotarajiwa kufanywa na Biden katika kufufua makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2018, yaliyofikiwa chini ya utawala wa Barack Obama.

Iran inaiyooshea kidole Israel, huku ikiamini kuwa mauaji hayo yana baraka za rais Trump anayeondoka.

Mshauri wa masuala ya kijeshi wa kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameapa kulipiza kisasi kikali kwa wauaji wa shahidi huyo. "Katika siku za mwisho za maisha ya kisiasa ya mshirika wao Trump, Mazayuni wanataka kuongeza shinikizo dhidi ya Iran na kuanzisha vita kamili," Hossein Dehgan aliandika kwenye twitter.

Waziri mkuu wa Israel, anakumbukwa kwa kumtaja mwanasayansi Fakhrizadeh alipozungumzia tuhuma dhidi ya Iran kuelekea mipango ya nyuklia.

Israel imekataa kuzungumza chochote. Ikulu ya White House, wizara ya ulinzi, Pentagon na wizara ya mambo ya kigeni pamoja na shirika la kijasusi la Marekani, CIA pia wamekataa kutamka chochote kuhusu mauaji hayo, ikiwa ni pamoja na timu ya mpito ya rais mteule Joe Biden.

Fakhrizadeh amekuwa akielezewa na mataifa ya magharibi na shirika la kijasusi la Israel kama kiongozi wa siri wa programu ya bomu la atomiki iliyosimamishwa mwaka 2003, na ambayo Israel na Marekani inasema Iran inajaribu kuirejesha. Iran hata hivyo inakana madai hayo.

Fakhrizadeh alikuwa mwanasayansi pekee wa Iran aliyeitwa katika "tathmini ya mwisho" ya shirika la kimataifa la nguvu za atomiki ya 2015, ya maswali ya wazi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Ripoti hiyo ilisema alisimamia shughuli "zilizounga mkono mwelekeo wa kijeshi kwa mpango wa nyuklia wa Iran ".

Lakini pia alikuwa ni mtu muhimu wakati waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alipokuwa akiwasilisha ripoti akiituhumu Iran kwa kuendelea kuzalisha silaha za nyuklia mnamo mwaka 2018.  "Kumbuka hilo jina, Fakhrizadeh," Netanyahu alisema kwenye mawasilisho hayo.

Post a Comment

0 Comments