Serikali yawataka wataalamu wake kutumia taaluma zao kuinua thamani ya mazao ya mifugo na uvuvi

 


WATAALAMU wa Mifugo wametakiwa kutumia taaluma zao na kushiriki kikamilifu katika kubuni mbinu za kisasa za kuinua viwango vya minyororo ya thamani ya mazao ya Mifugo na Uvuvi ili kuleta tija na kukidhi mahitaji ya uchumi wa viwanda kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.

Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Amos Zephania amesema hayo alipokuwa akifungua Kongamano la 43 la Kisayansi la Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Uvuvi na Mkutano wa 44 wa mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo Tanzania linalofanyika jijini Dodoma kuanzia Desemba 2- 4, 2020.

Zephania amesema kuwa Serikali imedhamiria kuanzisha na kuendeleza viwanda mbalimbali hususani vya uzalishaji na usindikaji wa mazao ya kilimo na mifugo ambavyo ni msingi wa maendeleo endelevu. 

“Serikali inatambua kuwa maendeleo ya viwanda hapa nchini yatachagiza upatikanaji wa bidhaa muhimu na bora kwa matumizi ya ndani na nje ya nchi jambo ambalo litainua ubora na viwango vya maisha ya wananchi, kujenga uchumi imara na kukuza uchumi wa Taifa unaoweza kuhimili ushindani wa kikanda na kimataifa,” Amesema Zephania.

Amesema kuwa ni wazi kwamba mifumo ya uzalishaji wa mifugo na uvuvi katika nchi yetu imeegemea zaidi katika uzalishaji kwa mifumo ya asili ambapo wazalishaji wengi ni wafugaji na wavuvi wadogo wadogo.

Ameongeza kuwa mifugo mingi iliyopo bado ni ya asili ambayo  tija katika uzalishaji wake hairidhishi huku akisema kuwa  ngómbe wengi wa asili wana uzito mdogo wa kati ya  kilo 200 hadi 350 ambao hupelekea kutoa maziwa kidogo na  nyama kidogo ambayo haizidi wastani wa kilo 175. 

Zephania amesema kuwa Wataalamu wa Mifugo wanajukumu la kufanya kuleta mabadiliko katika mifumo ili kuongeza ufanisi na tija ya uzalishaji kwa kutumia sayansi na teknolojia za kisasa huku akiwasisitiza  kuwasaidia wafugaji waweze kuongeza ubora wa uzalishaji ili  mali ghafi za uhakika ziweze kupatikana kwa matumizi ya  viwanda vya kusindika mazao ya mifugo na uvuvi.

“Huu ni wakati mwafaka wa kufanya mapinduzi makubwa katika minyororo ya thamani ya mifugo na samaki ili kukidhi mahitaji ya uchumi wa viwanda tunaouzungumzia kwa sababu mahitaji ya lishe ya protini inayotokana na mifugo yanatarajiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa katika miaka 20 ijayo kutokana na ongezeko la idadi ya watu, kukua kwa miji na kuongezeka kwa kipato cha watu,” Amesema Zephania.

“Hivyo ni lazima  uzalishaji wa mifugo na samaki  uboreshwe ili kukidhi mahitaji haya, wahimizeni wafugaji na wazalishaji kuwekeza katika teknolojia na vitendea kazi sahihi vitakavyowaongezea uzalishaji mashambani mwao na kuwawezesha kufikia masoko kwa ufanisi zaidi,”alifafanua Zephania

Aidha, Zephania aliwahimiza wataalamu hao kuendelea kuimarisha afya za mifugo, usimamizi wa mifumo bora ya uzalishaji na kutoa huduma za ugani kwa wakati sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya masoko ikiwemo uhifadhi, usafirishaji na usambazaji wa mazao hayo huku akisema kuwa mazao ya mifugo na uvuvi yanaharibika upesi yasipotunzwa na kuhifadhiwa ipasavyo.

Naye, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Maduka Kessy amesema kuwa jukumu la Wataalamu hao ni kuinua tija na faida kwa wafugaji wanaoshiriki katika uwekezaji kwenye mnyororo mzima wa thamani.

Kessy ameongeza kuwa Mkoa wa Dodoma una zaidi ya Kaya Mia nne na Hamsini Elfu (450,000) na kati ya kaya hizo Asilimia 44 ni wafugaji na ndio wenye kipato cha chini na maendeleo yao ni duni, hivyo kuna haja ya kuwaendeleza ili waweze kunufaika na mifugo yao.

“Dodoma ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kuwa na mifugo mingi, mpaka sasa takwimu zinaonesha tuna ng’ombe milioni 1.8 lakini mnyororo wa thamani kwa mifugo hiyo ni mfupi sana, hivyo kuwepo kwenu hapa leo ni faraja ya kwamba mtakuwa chachu ya mabadiliko kwa wafugaji wetu ili waweze kufaidika na mifugo yao,” Amesema Kessy.

Post a Comment

0 Comments