Biden aomba msamaha kwasababu ya wanajeshi kulala eneo la kuegesha magari


Rais Joe Biden wa Marekani ameomba msamaha baada ya baadhi ya wanajeshi waliokuwa wamewekwa kulinda eneo la Capitol kupigwa picha wakiwa wamelala katika eneo la kuegesha magari.

Zaidi ya wanajeshi 25,000 walipelekwa Washington DC kwa ajili ya kushughuli ya kuapishwa kwake mapema mwezi huu.

Picha walizopigwa maafisa hao zilianza kusambaa mtandaoni Alhamisi zikiwaonesha wakiwa wamepumzika katika eneo la karibu la kuegesha magari wabunge waliporejea.

Hali hiyo ilisababisha hasira miongoni mwa wanasiasa huku baadhi ya magavana wakawaondoa wanajeshi wao kwasababu ya utata huo.

Bwana Biden alizungumza na mkuu wa jeshi la kulinda usalama wa taifa Ijumaa, kuomba msamaha na kuuliza ni kipi ambacho kingekuwa kimefanywa kuweka mambo sawa, kulingana na vyombo vya habari vya Marekani.

Mama wa taifa Jill Biden pia naye alitembelea baadhi ya vikosi hivyo kuwashukuru akiwa amewabeba biskuti kutoka Ikulu kama zawadi.

"Leo hii nilitaka tu kuja na kuwashukuru kwa kutulinda mimi pamoja na familia yangu," alisema.

Wengi walianza kuzungumzia juu ya hali hiyo huku wanajeshi hao wakiwa wanapigwa na moshi wa magari wakiwa hawana uwezo wa kufikia maeneo muhimu kama choo baada ya kuwa katika hali ya tahadhari kwa siku kadhaa.

Kuna taarifa za kukanganya kuhusu kwanini wanajeshi hao walipelekwa Capitol lakini vikosi kadhaa walielezea vyombo vya habari kwamba agizo hilo liliwafikia Alhamisi mchana bila maelezo yoyote.

Picha hizo pia zimesababisha wasiwasi juu ya kusambaa kwa virusi vya corona miongoni mwa wanajeshi hao.

Afisa wa Marekani ambaye hakutaka kutambuliwa aliyezungumza na shirika la habari la Reuters Ijumaa, amesema kwamba kati ya wanajeshi 100 na 200 ya waliopelekwa eneo hilo walikuwa na virusi vya corona.

Baada ya picha hizo kuanza kusambaa, wabunge walionesha hasira zao kwenye mitandao ya kijamii huku wengine wakitoa ofisi zao kama sehemu ambazo wanaweza kupumzika.

Post a Comment

0 Comments