Jan 11, 2021

Jifunze kuishi ndoto yako kwa kufanya haya

 

Hakuna uhalisi wa mafanikio katika maisha ya mtu pasipo kuchukua hatua. Ili mtu aweze kufanikiwa katika maisha yake ni lazima ajifunze kuchukua hatua za kivitendo kila siku dhidi ya malengo na ndoto yake aliyonayo.

Kufanikiwa si jambo rahisi kivile kama watu wengi wanavyofikiri ila ni jambo linalohitaji uvumilivu na kujitoa kila siku kwa ajili kuhakikisha mafanikio yanatokea juu yetu.

Wapo watu wengi wanaotembea na malengo yale yale miaka na miaka pasipo kuchukua hatua yoyote dhidi yao na badala yake wamebaki na wimbo ule ule wa kusema “nitafanya kesho, nitampigia simu kesho, nitamtafuta ofisini kwake kesho, nitaenda kesho.” Wao kila kitu wanachopanga wamekuwa ni watu wasiochukua hatua bali kuimba wimbo wa kesho- kesho pasipo kuchukua hatua.

Kama unataka kufanikiwa katika maisha yako amua kuchukua hatua leo hii juu ya ndoto yako. Amua kuwasiliana na mtu unayetaka akusaidie juu ya kufanikisha malengo yako, amua kwenda ofisini kwa mtu unayemwitaji muda mrefu akuvushe mahali unapotaka, amua kurudi shule kuongeza ujuzi, amua kusimamia upya kipaji chako ili kiweze kukuingizia kipato, amua kusimamia msimamo wako wa kujiajiri. Kumbuka ndoto yako inawezekana kama utamua kuifata na kuitimiza.

Maisha yako ya kufanikiwa yanategemea sana hatua ndogo ndogo unazochukua kila siku. Usitake kufanikiwa kwa mara moja bali amua kuchukua hatua ndogo leo hii ili uweze kutengeneza mazingira ya kufanikiwa hapo kesho.

Hata mjenzi wa nyumba hakuanza moja kisha kesho akakamilisha nyumba na kuamia, bali alinzia kwenye kuchimba na kujenga msingi kisha akaanza kupanda hadi kwenye lenta kisha akaanza kuweka paa na kisha kukamilisha hatua zote za mwisho na hapo nyumba ikakamilika. Kila mafanikio tunayoyataka katika maisha yetu yana misingi na hatua zake ili kuweza kufikia kilele chake na kuwa halisi katika maisha yetu.

Nakusihi amua kuchukua hatua leo juu ya ndoto yako ili uweze kuona matokeo makubwa unayoyahitaji katika maisha yako. Kila mtu anakusubiri uchukue hatua ili uweze kuzaa matokeo yatakayokuwa na faida kwa kila mtu aliyekuzunguka. Kumbuka kadiri unavyochelewa kuchukua hatua juu ya ndoto yako ndivyo unavyozidi kuchelewa kufanikiwa zaidi katika maisha yako. Chukua hatua sasa.

Fanya zoezi hili kila siku:
1: Andika malengo 3 kila siku yakuchukua hatua juu yake.
2: Weka vipaumbele katika malengo hayo.
3: Orodhesha watu muhimu wa kukusaidia katika kufikia malengo yako.
4: Chukua hatua ndogo kila siku. Usisubiri ufanikishe kila kitu.
KWA HABARI, LIVE TV, RADIO, MATOKEO YA LIGI ZOTE DUNIANI DOWNLOAD APP YA MUUNGWANA BLOG <DOWNLOAD HAPA>
Share:
Loading...

Popular Posts

Copyright © MUUNGWANA BLOG | Powered by Blogger