Mkuu wa Mkoa Rukwa aagiza Lambalamba wasakwe

 


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo ameagiza kukamatwa kwa waganga wa kienyeji wanaopiga ramli chonganishi maarufu kama “Lambalamba” kwa kosa la kuwadanganya wananchi na kuwadhulumu mali zao.


Wangabo ametoa agizo hilo jana kwa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Justine Masejo kufuati kilio cha wananchi wa vijiji mbalimbali vya bode la Ziwa Rukwa wanaolalamika kutapeliwa fedha na mbalimbali na Lambalamba hao.


Alisema kuwa nchi hii haiwezi kuendeshwa kwa imani za kishirikina ambazo zinarudisha nyuma juhudi za wananchi katika kujikwamua na umasikini, hivyo kulitaka jeshi la Polisi kukiweka chini ya ulinzi Kijiji chochote kitakachoonekana kinawaficha waganga hao ama kutotoa ushirikiano kwa jeshi hilo.


Alisema anawashangaa wazazi wanaoshindwa kuwahudumia watoto wao kwa mahitaji ya shule ili wapate elimu, lakini wanatumia pesa kumpatia mganga wa kienyeji ili aweze kumsafishia mji wake (nyumba) kishirikina.


Aliongeza kuwa wazazi na wananchi wanaofanya vitendo kama hivyo wamejiroga wenyewe kwa kushindwa kujitambua.


“RPC anzisha msako kamata hawa lambalamba wote, bonde la Ziwa Rukwa kuanzia kule chini Kijiji cha Kasense mpaka kule Kilyamatundu (umbali km 174) kote kamata nimechoka kusikia malalamiko ya wananchi kila kukicha kudhulumiwa na kutapeliwa fedha,” alisema.


“Mnazidi kuwa masikini mnajiletea umasikini na wao walishajua kuwa ni wajinga hawa na wajinga ndio waliwao, wanakuja huku wanasema leta hela na wewe unatoa wakati una mahitaji ya msingi, nyumba yako familia yako umeitelekeza halafu unampelekea lambalamba hazikutoshi wewe, unapaswa hata kuombewa kabisa,” alisema.


Awali, Mkuu wa Wilaya Sumbwanga, Dk. Halfan Haule alisema pamoja na kuwa “Lambalamba” hao hawajafika katika baadhi ya vijiji wilayani humo, lakini kuna kamati ambazo zimeanza kuundwa kwa ajili ya mapokezi ya hao “Lambalamba”.


Maandalizi hayo yanakwenda sambamba na kuwachangisha fedha wananchi, ambao wanatumia fedha zao ambazo zingewafaa kwa maendeleo ya familia zao wanapeleka ili kupigwa ramli chonganishi.


Dk. Haule aliongeza kuwa waganga hao wanapitia kwenye ofisi za matawi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitisha fomu zao na kuwasainisha wananchi na kuwachangisha fedha kati ya Sh10,000, Sh1milioni.


Fedha ya maendeleo watakwambia hawana, lakini fedha kwa ajili ya kumleta Lambalamba hapa kila kaya inatafuta wanauza ng’ombe, mbuzi, juzi walipita kule (Kijiji cha Mawenzusi, Mwenyekiti wa Tawi wa CCM, Balozi na mwenyekiti wa kitongoji ndio waliowakaribisha.


“Tuliwakamata hapa wakati wanakuja kwa balozi, wale wanaoitwa Lambalamba ile kamati ya mapokezi hasa wale wazee wa mila na viongozi watakaowapokea au mwananchi tutawakamata haraka,” alisema.


Kaimu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa, Enos Budodi alisema kuwa hatawapokea wala kuwapa ushirikiano viongozi wote wa CCM watakaojihusisha na kuwapokea “Lambalamba” hao katika maeneo yao.


Imeandikwa na Mussa Mwangoka

Post a Comment

0 Comments