Mtu mmoja afariki baada ya wafuasi wa Trump kuvamia bunge


Polisi imethibitisha kuwa mwanamke mmoja aliyepigwa risasi wakati wa vurugu zilizotokea baada ya wafuasi wa Trump kuvamia bunge, amefariki dunia kwasababu ya majeraha aliyopata.

Bado maafisa hawajataja jina la mwanamke huyo lakini polisi wanasema alikuwa raia wa kawaida.

Aidha, mtu mwingine amepigwa risasi wakati wa vurugu zilizotokea ndani ya bunge la Marekani, kulingana na shirika la habari la Associated Press.

Lindsay Watts, mwanahabari wa shirika lenye kuhusishwa na Fox News, ameandika ujumbe kwenye Twitter kuwa wahudumu wa afya wa Washington DC walisema juhudi za kumuokoa mwanamke mmoja aliye kwenye hali mahututi zinaendelea baada ya kupigwa risasi kifuani.

Wafuasi wa Trump waliokuwa na hasira waliandamana huku wakiimba, "Tunamtaka Trump" huku mmoja wao akipigwa picha akiwa ameketi kwenye kiti cha rais wa bunge la Seneti.

Polisi Washington imesema kuwa ni wazi waandamanji hao walikuwa tayari kutumia nguvu yoyote ile kuingia katika majengo ya bunge.

Huku akiwa ameketi katika kiti cha spika wa bunge la wawakilishi Nancy Pelosi mmoja ya waandamanaji hao aliwacha ujumbe uliosema hatutakubali

Inasemekana hadi kufikia sasa watu 13 na silaha tano zimenaswa na polisi wakati ghasia zinaendelea bungeni.

Baada ya uvamizi huo uliochukua saa kadhaa, afisa anayesimamia mipangilio ya bungeni alitangaza kuwa sasa jengo hilo limenusuriwa na vikosi vya usalama.

Wakati mmoja Bwana Trump alilazimika kurekodi ujumbe kwenye video na kuutuma katika mtandao wa Twitter akitoa wito kwa wafuasi wake kuondoka katika majengo ya bunge lakini naye akawa anaendelea madai yasiokuwa na ushahidi wowote kuwa Democrats waliiba kura.

Lakini kukawa na ishara kidogo zinazoonesha kwamba waandamanaji hao wanatii wito wa Trump unaowataka warejee nyumbani licha ya kwamba mji huo wote unatekeleza hatua ya kutoka nje kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi kumi na mbili asubuhi.

"Najua machungu yenu, najua mumevunjika moyo," Trump alisema. "Lakini lazima sasa murejee nyumbani, lazima tuwe na amani ... hatutaki yeyote ajeruhiwe."

Bwana Biden kwa upande wake amesema maandamano hayo "yamesababishwa na uchochezi na ni lazima hilo likome sasa", amesema.

Wanajeshi na maafisa wa polisi pia wamepelekwa katika majimbo jirani huku maafisa wa shirika la ujasusi FBI wakipelekwa katika majengo ya bunge kusaidiana na maafisa wa polisi.

Post a Comment

0 Comments