Wafanyabiashara Mlandizi wataka soko lao liboreshwe


Na Omary Mngindo, Mlandizi

WAFANYABIASHARA katika soko la Mlandizi lililopo Kata ya Janga halmashauri ya wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani wameuomba uongozi wa halmashauri hiyo kuendelea kuliboresha soko hilo ili wafanye shughuli zao kwa uhakika zaidi.

Aidha wameanza kuushukuru uongozi huo, wa soko, wafanyabiashara wenzao kwa kuchangia ujenzi huo akiwemo mbunge aliyemaliza muda wake, kwa kushirikiana katika kujenga soko hilo ambalo kwa sasa limeshapauliwa hali inayowaondolea kero ya kuvujiwa pindi mvua inaponyesha.

Wakizungumza kwa niaba ya wenzao sokoni hapo, Idd Adam, Isawa Mkindi, Victor Bilali na Maryamu Msuya walisema kuwa kwa sasa wanafanyabishara zao kwa raha kwani hata mvua ikinyesha hakuna adha ya vibanda vyao kuvuja wala matope yaliyokuwa yanasababishwa na maji yaliyokuwa yanatuhama saokoni hapo.

“Pamoja na kuwashukuru viongozi wetu ngazi mbalimbali, lakini tunawaomba watuboreshee kwa kuweka sakafu ya zege hapa chini ili kutondolea vumbi, pia kuna wenzetu ambao wapo nje ya haya mabati ambao mvua inaponyesha wanafunga biashara zao na kukimbilia eneo hili,” alisema Adam.

Kwa upande wake mmoja wa wateja aliyezungumza na waandishi sokoni hapo aliyejitambulisha kwa jina la Mkindi alisema kwamba wafanyabiashara waliopo nje ya jingo hilo wanaolalamika kunyeshewaa na mvua, wanaweza kuingia ndani ya eneo hilo lililohezekwa endapo halmashauri itatengeneza meza badala ya zilizopo sasa kujengwa kiholela holela na wafanyabiashara wenyewe ambazo kila mmoja ameitengeneza kwa ukubwa tofauti.

“Halmashauri ikijenga meza kwa mfumo mmoja utaokoa maeneo makubwa yaliyotumika vibaya kutokana na utengezaji wa meza kila mmoja binafsi, ujenzi wa meza kwa mfumo mmoja pia utapunguza njia na ukubwa wa meza hizo, hivyo wote watakuwa ndani ya mfumo uliopo hivi sasa kwa maana ya ndani ya jingo hili lenye paa kubwa,” alisema Mkindi.

Kwa upande wake Maryamu alisema soko hilo kwa sasa japokuwa halijamalizika lakini angalau limeondoa adha ambayo awali wafanyabiashara hao walikuwa wanaipata, huku akiomba kuwekwa mfumo wa umeme utaowawezesha kuwepo kwa sehemu za kuchajia simu.

Post a Comment

0 Comments