Kituo cha afya Makambako chawatoza shilingi 4000 watoto chini ya miaka 5 ili kumuona daktari


Brigither Nyoni na Amiri Kilagalila,Njombe

Wananchi mjini Makambako wameiomba serikali kutoa  ufafanuzi kuhusiana na  mabadiliko ya utoaji wa huduma za afya katika kituo cha afya Makambako baada ya watoto chini ya miaka mitano kutakiwa kulipia fedha ili waweze kupatiwa matibabu.

Wakizungumza na mwandishi wetu baadhi ya wanawake mjini Makambako  wamesema kuwa awali watoto wenye umri chini ya miaka mitano walikuwa wanatibiwa bure lakini kwa sasa wanaambiwa walipe elfu nne ili wapatiwe huduma.

Akizungumza kwa niaba ya mganga mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, FROLA MDUGO amekiri kutokea kwa mabadiliko hayo na kueleza kuwa kwa sasa watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanatakiwa kulipia elfu nne ambayo ni Kwa ajili ya kumuona daktari  lakini upande wa vipimo na dawa watapatiwa bure.

Hata hivyo amesema kuwa kwa wanawake wajawazito kwa sasa watapatiwa matibabu bure endapo watakuwa na tatizo la afya linalohusiana na ujauzito lakini kama watakuwa na tatizo la kiafya ambalo halihusiani na ujauzito wanatakiwa kulipia matibabu yote.

Sera ya Afya nchini Tanzania  inataka huduma za Afya kwa wazee, wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano kupata bure, lakini kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya makundi hayo  kutokana na kutozwa fedha za matibabu.

Post a Comment

0 Comments