Mtoto Wa Miaka Minane Apata Ujauzito

 


KATIKA hali isiyo ya kawaida mwanafunzi mwenye miaka minane anayesoma darasa la pili katika shule mojawapo ya msingi wilayani Missenyi mkoani Kagera amepewa ujauzito.


Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya Missenyi, Beatrice Sanga alisema kuna kesi nane za mimba katika shule za msingi mojawapo ndani ya Wilaya ya Missenyi. Wanawapima watoto ujauzito kila baada ya miezi mitatu.


Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya Missenyi, Lucy Eustace alisema mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minane anaweza kubeba mimba endapo yai litakuwa limekomaa na mji wa uzazi umejiandaa kwa ajili ya kupokea mtoto iwapo atakutana na mwanaume.


Alisema taarifa za hospitali zimethibitisha mwanafunzi huyo (jina limehifadhiwa) ni mjamzito. “Najua hii inashangaza wengi lakini lazima mtambue kuwa ni mara chache mtoto wa miaka minane kubeba ujauzito ingawa mtoto anaweza kupata mimba kama yai limekomaa na mji wa mimba umejiandaa kupokea mtoto,”alisema Eustace.


Wilaya ya Missenyi ina idadi ya wanafunzi 53,617 wa shule za msingi na wanafunzi wa sekondari 11,637.


Sanga alisema mbali na tatizo la mimba kujitokeza katika shule za halmashauri ya Missenyi lipo tatizo la maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa watoto ambapo katika kata tano kati ya kata 20 zilizoko wilayani Missenyi jumla ya wanafunzi 175 wa shule ya msingi wamegundulika kuwa na maambukizi ya Ukimwi huku kata nyingine 15 zikitizamiwa kupimwa maambukizi ya virusi hivyo.

Post a Comment

0 Comments