Mahakama ya Wilaya ya Serengeti imemhukumu mkazi wa kijiji cha Nyakomogo, Joma Masoya (34) kutumikia kifungo cha miaka 20 jela baada ya kumtiwa hatiani kwa kukutwa na vipande vinne vya nyumbu.
Katika
hukumu iliyosomwa leo Ijumaa Julai 30, 2021 na Hakimu Mkazi wa Wilaya,
Judith Semkiwa katika kesi ya Uhujumu Uchumi namba 55/2020 mshitakiwa
ametiwa hatiani kwa makosa matatu aliyoshitakiwa nayo.
Hakimu
Semkiwa amesema katika kosa la kuingia kwenye hifadhi bila kibali adhabu
yake ni mwaka mmoja, kukutwa na silaha hifadhini adhabu yake ni miaka
miwili na kukutwa na nyara za Taifa adhabu yake ni kifungo cha miaka 20
gerezani.
Mapema mwendesha mashitaka wa Jamhuri, Jakobo
Matatala aliiambia mahakama kuwa mshitakiwa alikamatwa Julai 12, 2020
katika milima ya Kirawila ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kinyume
na sheria.
Amesema alifikishwa mahakamani kwa kosa la kuingia
hifadhini bila kibali, kukutwa na silaha za jadi hifadhini bila kibali
na kukutwa na vipande vinne ambavyo ni sawa na nyumbu mzima bila kibali
na kuomba mahakama kutoa adhabu kali.
Mshitakiwa ameomba apunguziwe adhabu kwa kuwa anategemewa na familia.
0 Comments