Mtoto wa nyota wa zamani wa Man Utd na England aanza kukipiga Fort Lauderdale

Romeo Beckham, mtoto wa nahodha wa zamani wa England David Beckham, Jumapili hii amecheza mchezo wake wa kwanza akiwa na timu ya Fort Lauderdale inayoshiriki ligi daraja la tatu nchini Marekani.

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 19 alianza kama kiungo, nafasi aliyokuwa anaichezea baba yake kwenye mchezo wa sare ya 2-2 dhidi ya South Georgia Tormenta.

Timu hiyo ni ya akiba iliyo chini ya timu ya Inter Miami – inayoshiriki ligi kuu ya Marekani na inayomilikiwa na baba yake.

"Ni Baraka kucheza mchezo wangu wa kwanza wa kulipwa usiku huu," Romeo aliandika katika mtandao wake wa Instagram.

Romeo aliyesaini mkataba wa kulipwa na klabu hiyo mapema mwezi Septemba, alionyesha mchezo mzuri na kutengeneza nafasi muhimu ya kufunga mwanzoni mwa mchezo huo.

Katika sehemu ya kiungo kulikuwa na muunganiko mzuri akicheza sambamba na Harvey Neville, mtoto wa kocha mkuu wa Inter Miami, Phil Neville. Phil Neville alicheza pamoja na Beckham kwenye klabu ya Manchester United.

Mtoto wa Neville alikuwa akicheza mchezo wake wa 16 akiwa na timu hiyo yenye maskani yake huko Florida, baada ya kuondoka kwenye timu ya vijana ya Manchester United na kujiunga na baba yake nchini Marekani.

Romeo Beckham alipumzishwa katika dakika ya 79 na kusema kwa sasa "mawazo yake yote ni kwenye mchezo unaofuata".

Baba yake Beckham alitikisa vichwa vya habari duniani baada ya mwaka 2007 kufanya uhamisho wa kushangaza wa kuhamia LA Galaxy ya Marekani akitokea kwa magwiji Real Madrid.

Akiwa Marekani alishinda vikombe viwili mfululizo vya MLS mwaka 2011, 2012 na mwaka 2019 akajengewa sanamu nje ya uwanja wa La Galaxy ili kumpa heshima ya kuichezea klabu hiyo kwa miaka 6.

 

Post a Comment

0 Comments